IQNA

ISESCO yalaani uvunjiwaji heshima misikiti Uingereza

17:25 - June 18, 2011
Habari ID: 2139930
Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Jumuiya ya Nchi za Kiislamu ISESCO limetoa taarifa likilaani uvunjiwaji heshima misikiti na makaburi ya Waislamu nchini Uingereza pamoja na kuongezeka vitendo vya chuki dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo.
Isesco imetoa taarifa hiyo baada ya kuwasilishwa kwake ripoti ya Baraza la Waislamu wa Uingereza ambayo inasema kuwa vitendo vya dharau na chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu vimeongezeka sana nchini humo katika kipindi cha mwaka huu na uliopita.
Ripoti hiyo pia imesema kuwa mashambulio ya kibaguzi yaliongezeka dhidi ya Waislamu, makaburi na maimamu wa misikiti ya Uingereza katika kipindi cha mwaka uliopita na kuitaka ISESCO ichukue hatua za dharura ili kukabiliana na jambo hilo.
Ripoti hiyo imesema kuwa kutupwa nyama za wanyama walioharamishwa kuliwa na Uislamu kwenye maeneo ya misikiti na vilevile kuandikwa maandishi ya chuki na ubaguzi kwenye kuta za misikiti hiyo ni baadhi ya hatua za kibaguzi zilizotekelezwa dhidi ya Waislamu mwaka uliopita.
Baraza la Waislamu wa Uingereza limesema kuwa kesi 1200 za mashambulio kama hayo ya kibaguzi dhidi ya Waislamu ziliripotiwa mwaka uliopita wa 2010. Kuhusu jambo hilo, Isesco imewataka viongozi wa Uingereza kuchukua msimamo wa wazi na kukemea vitendo hivyo vya kusikitisha dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo na vilevile kuchukua hatua za dharura kwa lengo la kuwafikishwa mahakamani wahalifu wanaohusika na vitendo hivyo. 809901
captcha