Hatua hiyo imefanyika wakati umebaki muda mfupi kabla ya kuanza kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani ili kuondoa tofauti zilizopo kwa Waislamu katika kuanza na kumaliza mwezi huo.
Mtunzi wa kitabu hicho, Profesa Juma Mikidadi alisema kitabu hicho kimeelezea muandamo wa mwezi kijiografia pamoja na masuala mengine huku akieleza hadithi mbalimbali kuhusu suala hilo.
Akielezea hilo, Shehe huyo mwenye shahada mbili za elimu ya dini, alisema pande mbili zinasimamia kufunga na kufungua kwa kuuona mwezi, lakini bado kuna tofauti.
“Wakati huu dunia inaungana hata Afrika sasa inapanga kuwa na nchi moja ni kwa nini Waislamu ambao hatuna mipaka, tumeguke vipande vipande hasa katika ibada? Ni lazima tuungano na kuwa wamoja kuhakikisha suala hili linafikia tamati,” alisema Shekhe Profesa Mikidadi aliyewahi kuwa Mbunge wa Kibiti mkoani Pwani kuanzia mwaka 1995 hadi 2000.
Naye mwanazuoni mwingine wa Tanzania Shekhe Mohamed Iddi Mohamed alisema tatizo hilo ni la dunia nzima siyo Tanzania pekee .
Akizindua kitabu hicho, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi alisema kitabu hicho kitasaidia Waislamu kuondoa tofauti zao katika suala hilo lililodumu kwa muda mrefu.
Aidha, alisema Waislamu wanatakiwa kutambua kutofautiana katika masuala mbalimbali siyo kugombana kwa suala hilo likiachwa kukua, linaweza sababisha ugomvi baina ya Waislamu kama ilivyo katika nchi nyingine kwa kurusha mabomu misikitini.
Dk. Mwinyi alinunua vitabu 300 kwa ajili ya maimamu wote wa Mkoa wa Dar es Salaam ili kuelewa jambo hilo na kuwaelezea waumini wao.
827838