Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu:
Mwamko wa Kiislamu unaoshuhudiwa sasa ni tukio kubwa mno
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, mwamko wa Kiislamu unaoshuhudiwa hivi sasa Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika ni tukio kubwa mno ambalo halijawahi kushuhudiwa tangu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.
Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei amesema hayo wakati alipokutana na viongozi na maafisa mbalimbali wa serikali na kusisitiza kuwa, nukta ya kwanza chanya ya mfumo wa Kiislamu nchini Iran ni kuthibitisha mfumo huu kwamba una uwezo wa kukabiliana na vitisho vya maadui. Kiongozi Muadhamu ameongeza kuwa, katika kipindi chote cha miaka 32 ya baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, taifa la Iran limekabiliwa na vitisho mbalimbali vikiwemo vya kisiasa, kiusalama, kijeshi na kiuchumi; lakini kusimama kwake kidete kumelifanya liweze kushinda vitisho vyote hivyo.
Ayatullah Khamenei aidha amesema kuwa, moja ya sifa nyingine muhimu ya mfumo wa Kiislamu ni kufanikiwa kupata maendeleo katika kipindi kigumu cha kuwekewa vikwazo. Amebainisha kwamba, maendeleo yamepatikana hapa nchini kutokana na hali ya kujiamini ambayo ni ya kitaifa. 839148