IQNA

Sheikh wa al Azhar:

Mashia hawana Qur'ani tofauti ya ile ya Masuni

16:06 - August 20, 2011
Habari ID: 2174076
Sheikh wa al Azhar nchini Misri amesema katika ufunguzi wa Mashindano ya 19 ya Kimataifa ya Qur'ani nchini Misri kwamba baadhi ya kanali za televisheni zinafanya njama za kudhihirisha kwamba Qu'ani ya Mashia inatofautiana na ile ya Masuni na kwamba madai hayo ni urongo mtupu unaotaka kuzusha fitina.
Sheikh Ahmad al Tayyib amesema kuwa Qur'ani Tukufu ya Waislamu wote ni moja na Waislamu wote wa madhehebu ya Shia na Suni wanakubali kitabu hicho kitukufu wala hakuna tofauti baina yao.
Amesema madai yanayotolewa na baadhi ya kanali za televisheni kwa ajili ya kuonyesha tofauti kati ya eti Qur'ani ya Mashia na ile ya Masuni hayana ukweli wowote na yanatolewa kwa lengo la kuanzisha moto wa fitina baina ya Waislamu na kufikia malengo ya kisiasa.
Sheikh wa al Azhar amesisitiza kuwa Qur'ani Tukufu ndiyo marejeo ya Mashia na Masuni na amewataka Waislam wote kufanya juhudi za kutadabari na kuzama ndani ya kitabu hicho na kutotosheka na hifdhi na kusoma aya zake tu.
Sheikh wa al Azhar aliyasema hayo wakati wa kufungua Mashindano ya Kimataifa ya Hifdhi, Tajwidi na Tafsiri ya Qur'ani nchini Misri yaliyoanza Alkhamisi iliyopita katika Chuo Kikuu cha al Azhar mjini Cairo. 846673



captcha