Duru ya 24 ya mashindano ya kimataifa ya Qur'ani Tukufu na Hadithi, maalumu kwa vijana wa nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi, yameanza leo Jumatatu nchini Kuwait.
Mashindano hayo yamepangwa kuendelea kwa muda wa siku nne.
Kwa mujibu wa gazeti la al-Qabas linalochapishwa nchini humo, Yusuf as-Saidi, Mkuu wa kamati kuu inayosimamia mashindano hayo amesema kuwa mashindano hayo yanafadhiliwa na Shirika la Kitaifa la Michezo na Vijana la Kuwait PAYS na kwamba vijana washiriki wanachuana katika vitengo tofauti vya hifdhi na kiraa ya Qur'ani Tukufu na Hadithi za Bwana Mtume (saw).
As-Saidi amesema mashindano hayo ambayo yanasimamiwa na waamuzi 6 kutoka nchi zilizotajwa yanafanyika katika nyakati mbili tofauti za asubuhi na alasiri.
Washiriki 54 kutoka nchi sita wanachama wa baraza lililotajwa la ushirikiano watachuana katika makundi matatu ya umri tofauti wa miaka 10 hadi 14, 15 hadi 18 na 19 hadi 25. 867306