IQNA

14:33 - October 13, 2011
Habari ID: 2204180

Polisi ya New York yaonywa dhidi ya kuendelea kuwajasusi Wanachuo wa Kiislamu

Wahadhiri wa Chuo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha mji wa New York nchini Marekani (CUNY) wametoa taarifa wakiionya polisi ya mji huo dhidi ya kuendelea kufanya ujasusi dhidi ya wanachuo wa Kiislamu na kusisitiza kwamba jambo hilo linakwenda kinyume na sheria zinazopasa kulinda raia wa nchi hiyo.

Wahadhiri hao wametoa taarifa hiyo katika hali ambayo siku chache zilizopita baraza la chuo kingine cha Brookline lilitoa taarifa kama hiyo likiwaonya polisi hao dhidi ya kufanya ujasusi dhidi ya wanachuo wa Kiislamu.
Polisi ya New York imekuwa ikitumia makachero wake kupenya na kuingia kwenye safu za wanachuo wa Kiislamu na kisha kufanya ujasusi dhidi yao, ikiwa ni pamoja na kuchunguza shughuli zao za kila siku na kufuatilia mitandao wanayoitembelea.
Hiyo ni sehemu ya ujasusi mkubwa ambao polisi ya New York imekuwa ikiufanya dhidi ya jamii ya Waislamu wa mji huo ambapo imekuwa ikifuatilia na kukusanya habari na picha za shughuli zao za kila siku, yakiwemo maduka wanakonunua bidhaa na vyakula vya matumizi yao. Wataalamu wa mambo wanasema kuwa ujasusi unaofanywa na polisi ya New York dhidi ya wanachuo wa Kiislamu unakwenda kinyume na mapatano yaliyotiwa saini kati ya polisi hiyo na vyuo vikuu vya mji huo miaka 19 iliyopita.
Chuo Kikuu cha Mji wa New York, au kwa jina jingine City University of New York ndicho chuo kikuu kikubwa zaidi katika mji huo na kina zaidi ya wanachuo 480,000 na vyuo pamoja na taasisi za kielimu zipatazo 23. 878578
captcha