IQNA

Marekani inachochea fitina kwa kuituhumu Iran

17:56 - October 15, 2011
Habari ID: 2205226
Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya mjini Beirut Lebanon ametahadharisha juu ya athari hasi za kuituhumu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwamba imehusika na njama ya kutaka kumuua balozi wa Saudi Arabia mjini Washington Marekani na kusisitiza kwamba Marekani inataka kuzusha fitina na mifarakano kati ya nchi za Kiislamu kupitia tuhuma hizo.
Akizungumza hapo jana katika Msikiti wa Hassanein (as) mjini humo, Sayyid Ali Fadhlullah amesema kuwa Marekani imebuni njama na tuhuma hizo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ili kuishinikiza kisiasa kutokana na msimamo wake thabiti wa kuunga mkono masuala ya Kiislamu duniani na hasa kuhusu suala la Palestina.
Sayyid Fadhlullah ametaka Waislamu kuwa macho na watulivu mbele ya tuhuma hizo na kuongeza kuwa nchi za Kiislamu wakati huu zinapasa kuimarisha ushirikiano na uhusiano wao ili kuvunja njama za maadui wa Uislamu dhidi yao.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Fadhlullah amelaani vikali jinai na unyama wa utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina pamoja na kuongeza ujenzi wa vitongoji vya Mayahudi katika ardhi za Palestina.
Amesema utawala huo ghasibu umekuwa ukikanyaga matukufu ya Kiislamu bila kujali na kuikosoa jamii ya kimataifa kutokana na kimya chake mbele ya jinai na ukiukaji huo. Amesema inasikitisha kuona kwamba mamia ya Wapalestina wamekuwa wakiishi kwa miaka mingi katika ukandamizaji na mateso ya utawala huo bila ya Israel kuchukuliwa hatua zozote za kisheria.
Sayyid Ali Fadhlullah ameashiria mapatano ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas ya kubadilishana mateka na utawala haramu wa Israel na kuongeza kuwa ushindi huo mkubwa kwa Hamas ni kielelezo kinachothibitisha kwamba njia pekee ya kujikomboa Palestina ni kupitia mapambano. 879763
captcha