IQNA

Mapinduzi ya Misri yamesimama juu ya msingi wa kuhuisha dini katika jamii

16:37 - October 17, 2011
Habari ID: 2206653
Huku akiashiria nafasi muhimu ya dini katika jamii ya Misri, Sheikh Ahmad Tayyib wa al-Azhar amesisitiza kwamba mapinduzi ya watu wa nchi hiyo yamefanyika kwa lengo la kuhuisha nafasi muhimu ya dini katika nchi hiyo.
Sheikh Tayyib aliyasema hayo jana Jumapili alipokutana na kuzungumza na kundi la wasomi wa Misri na kusisitiza kuwa dini ni kiungo muhimu cha jamii ya nchi hiyo, kiungo ambacho amesema kilikuwa kimesahaulika katika siku za huko nyuma. Amesisitiza kwamba hakuna mapinduzi yoyote yanayoweza kutokea nchini humo bila ya kuzingatia utamaduni wa kidini wa Wamisri.
Sheikh Tayyib amesema kwa bahati nzuri makundi yote ya kisiasa ya Misri yametambua jambo hilo na kuliweka katika mipango ya shughuli zao.
Ameashiria pia umuhimu wa misikiti na taasisi za kidini katika jamii ya Misri na kuwataka maimamu na wahubiri wa nchi hiyo kulingania umoja na kujiepusha na masuala yanayosababisha mifarakano katika jamii.
Sheikh huyo wa al- Azhar amesema kuwa jukumu kubwa zaidi la wanafikra na wasomi wa Misri litakuwa ni kuimarisha fikra za waliowengi nchini kuhusiana na misingi na thamani za mafundisho ya Kiislamu. 881377
captcha