IQNA

Uislamu kuwa msingi wa kutungwa katiba ya Tunisia

22:50 - November 03, 2011
Habari ID: 2216865
Kiongozi wa chama cha Kiislamu kilichoshinda uchaguzi wa hivi karibuni nchini Tunisia cha an-Nahdha amesisitiza kwamba sheria za Kiislamu zitapewa umuhimu mkubwa katika utungaji wa katiba ya nchi hiyo ya Kiislamu.
Rashid al-Ghanushi amesisitiza kwamba kwa mtazamo wa chama chake hakuna mgongano wowote uliopo kati ya Uislamu na mantiki halisi ya mwanadamu wala kati ya Uislamu na misingi ya kielimu, ukisasa wala demokrasia halisi.
Kiongozi wa chama cha an-Nahdha ambacho kilipata ushindi mkubwa katika uchaguzi uliofanyika nchini Tunisia baada ya kung'olewa madarakani dikteta Ali Zeinul Abideen ametangaza kuwa hakuna mgongano wowote kati ya mafundisho ya Kiislamu na thamani za utu na kwamba Uislamu unathamini sana maslahi ya kiutu na uadilifu popote pale unapoonekana, hata kama hautakuwa na alama ya Uislamu moja kwa moja.
Akikanusha madai kwamba chama chake kinataka kuunda mfumo wa kiliberali na kisekula nchini Tunisia, al-Ghanushi amesema kuwa kamwe serikali ijayo haitapinga misingi na mafundisho ya kidini na kwamba serikali yake itafanya juhudi kubwa za kubuni mfumo wa Kiislamu na Kiarabu.
Ameongeza kuwa serikali yake ndiyo itakayokuwa ya kwanza kubuni mfumo wa aina hiyo wa Kiislamu baada ya kuanguka dikteta huyo wa zamani. Amesema hakuna udharura wa kuanzishwa mfumo wa kisekula katika nchi yoyote ya Kiislamu ili kuheshimu mfumo wa demorasia na haki za wachache kwa sababu jambo hilo tayari linadhaminiwa na Uislamu, tena kwa njia bora zaidi. 892277
captcha