Bendera ya taifa la Palestina itapeperushwa wiki ijayo katika makao makuu ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) katika sherehe maalumu, ikiwa ni ishara ya kukubalika nchi hiyo ya Kiarabu na Kiislamu kama mwanachama mpya wa shirika hilo muhimu.
Irina Bokova, Katibu Mkuu wa UNESCO na mabalozi wa nchi wanachama wa shirika hilo wanatazamiwa kushiriki kwenye shehere hiyo ambayo imepangwa kufanyika siku ya Jumanne tarehe 13 Disemba. Mahmoud Abbas na Riyadh Maliki, Rais na Waziri wa Mambo ya Nje wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kwa utaratibu pia wanatazamiwa kushiriki kwenye sherehe hiyo.
Palestina ilipata uanachama katika shirika la UNESCO kwa kupata kura 107 za ndio, 14 za hapana na wanachama 52 kujizuia kupiga kura.
Marekani ambayo kabla ya kupigwa kura hiyo iliitishia UNESCO kwamba ingekata mchango wake wa kifedha kwa shirika hilo kama lingekubali uanachama wa Palestina ilitekeleza kivitendo tishio hilo baada ya kura na hivyo kulinyima shirika hilo sehemu kubwa ya pato lake la kifedha. 912178