Hii ni mara ya pili katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita kwa makundi ya wabaguzi kuvamia na kuyavunjia heshima makaburi hayo ya St. Michel katika mji wa Carcassonne kusini mwa Ufaransa.
Baada ya kubomoa na kuharibu makaburi ya Waislamu wabaguzi wa rangi hao waliandika juu yake nara za chuki na ubaguzi dhidi ya Waislamu zikiwemo zile zinazodai kwamba Ufaransa ni ya Wafaransa pekee na kwamba Waislamu wanapasa kufukuzwa nchini humo. Walichora pia juu ya makaburi hayo yaliyoharibiwa alama za misalaba iliyovunjika.
Akizungumza mara tu baada ya kuzuru makaburi hayo yaliyoharibiwa na wabaguzi wa rangi wa Ufaransa, Abdullah Dhikri, Mkuu wa Baraza la Waislamu wa eneo hilo amesema kuwa Waislamu wote waliozikwa kwenye makaburi hayo walipigana Vita vya Kwanza vya Dunia kutetea ardhi ya Ufaransa na kwamba kuwavunjia heshima kwa kuwatendea vitendo hivyo vya dharau ni kuvunjia heshima taifa zima la Ufaransa.
Amesema vitendo vya ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya Waislamu wa Ufaransa vimeongezeka kwa kiwango cha kutisha katika miezi ya hivi karibuni kwa kadiri kwamba vimeongezeka kwa asilimia 30 katika mwaka huu tu ikilinganishwa na miaka iliyopita.
Bwana Dhikri amesema katika sehemu nyingine ya matamshi yake kwamba katika mwezi uliopita wa Novemba pekee mikisiti 6 muhimu iliteketezwa moto katika sehemu tofauti za Ufaransa na kesi 135 za chuki na ubaguzi dhidi ya Waislamu kuwasilishwa katika mahakama za nchi hiyo. 923495