IQNA

Mufti Mkuu wa Syria katika Mkutano wa Umoja wa Kiislamu Tehran:

Shia na Suni wanashiriki katika mwamko wa Kiislamu kwa nara ya Allahu Akbar

16:39 - February 08, 2012
Habari ID: 2271470
Waislamu wote wa Kishia na Kisuni wanashiriki katika mwamko wa Kiislamu na wanaeleza matakwa yao kwa kutumia nara ya Allahu Akbar bila taasubi za kimadhehebu.
Hayo yamesemwa leo na Mufti Mkuu wa Syria Ahmad Badruddin Hassun katika kikao cha kufungua Mkutano wa 25 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu unaofanyika mjini Tehran. Amesema kuwa siku hizi zinasadifiana na sikuukuu za kukumbuka tukio la kuzaliwa Mtume Muhammad (saw) na mjukuu wake Imam Swadiq (as), Mtume ambaye aling’oa mizizi ya utamaduni wa kijahilia na itikadi potofu za zama hizo na kuleta ujumbe wa kibinadamu akiwa rehma kwa walimwengu wote.
Mufti Mkuu wa Syria amesema kuwa kuzaliwa kwa Mtume (saw) kumesadifiana na siku ya kuzaliwa Imam Ja’far Swadiq ambaye alikuwa khalifa wa babu yake na shakhsia aliyelea wanafunzi wengi wa Kishia na Kisuni wakiwemo Abu Hanifa na Imam Shafi’ ambao ni miongoni mwa viongozi wakuu wa madhehebu za Kisuni.
Sheikh Badruddin Hassun amesisitiza juu ya udharura wa kuimarisha umoja wa Kiislamu na kusema : “Kabla ya kuwa Shia au Suni ni sisi sote ni Waislamu, na kwa msingi huo kuna udharura wa kuimarisha zaidi umoja wetu wa Kiislamu.”
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake Sheikh Badruddin Hassun amezungumzia propaganda chafu zinazofanywa na maadui dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema hii leo maadui wa Uislamu wanaendesha hujuma kubwa na kuchochea fikra za walimwengu dhidi ya Iran kwa sababu Jamhuri ya Kiislamu imekataa kuwa pamoja na mabeberu hao na kuamua kuwasaidia wanaodhulumiwa duniani.
Mufti wa Syria ametahadharisha kuhusu njama zinazofanywa na maadui wa Uislamu dhidi ya mataifa ya Kiislamu na akasema mabeberu hao hawakuketi kimya na wanafanya njama za kuanzisha hitilafu na migawanyiko katika nchi za Misri, Libya, Tunisia, Bahrain na kwengineko na kuzusha vita na umwagaji damu kati ya ndugu Waislamu na hatimaye kuzima mwamko wa sasa wa Kiislamu. 950162
captcha