Ismail Hania, Waziri Mkuu wa serikali halali ya Palestina amesema kuwa, serikali yake imesimama kidete mbele ya vitisho na mashinikizo yote ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Hania ambaye yupo hapa Iran na ambaye ameshiriki katika maandamano ya kuadhimisha miaka 33 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo katika hotuba yake mbele ya hadhara kubwa ya mamilioni ya Wairani kwenye Medani ya Azadi na kusisitiza kwamba, serikali halali ya Hamas inaiunga mkono kikamilifu Jamhuri ya kiislamu ya Iran.
Waziri Mkuu wa serikali halali ya Palestina ameashiria kusimama kidete wananchi wa Palestina mbele ya mashinikizo ya kila upande ya utawala wa Kizayuni wa Israel na kubainisha kwamba, kusimama kidete Wapalestina ndiko kulikowafanya wananchi hao madhulumu waushinde mzingiro, walishinde jeshi la Israel katika vita vya siku 22 na waibuke na ushindi pia katika ubadilishanaji mateka baina yao na Wazayuni. Amesisitiza kwamba, katu Hamas haitoitambua Israel ambayo ni dola ghasibu.
Safari ya Ismail Hania nchini Iran imefanyika huku baadhi ya nchi kama vile Kuwait na Qatar zikiwa zimefanya juhudi kubwa bila mafanikio za kuzuia safari ya Waziri Mkuu huyo wa Palestina nchini Iran.
951260