IQNA

Kituo cha Kiislamu cha Kuwait Chalaani uchomaji moto Qur'ani

17:04 - March 04, 2012
Habari ID: 2285407
Kituo cha Kiislamu cha Kuwait cha 'Wadhakkir' kimetoa taarifa kikilaani vikali uchomaji Qur'ani uliofanywa hivi karibuni na askari wa Marekani walioko nchini Afghanistan.
Kwa mujibu wa gazeti la ar-Rai la nchini Kuwait kituo kilichotajwa cha Kiislamu kimetoa taarifa kikisema kuwa Qur'ani si kitabu kitakatifu kwa Waislamu wa Afghanistan tu bali kwa Waislamu wote duniani na kwa hivyo kinapasa kuheshimiwa na kila mtu. Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa licha ya kuwa kuna baadhi ya watu waovu wanaokivunjia heshima kitabu hicho kitakatifu lakini kitadumu milele katika jamii ya mwanadamu kwa sababu kinalindwa na Mwenyezi Mungu mwenyewe. Imesema maadui wamekilenga kitabu hicho kitakatifu kwa sababu wanakichukulia kuwa hatari kubwa kwa maslahi yao haramu duniani. Kituo cha Kiislamu cha Wadhakkir kimesema kuwa Waislamu wamelengwa na hujuma kubwa ya maadui na kwamba wanapasa kushikamana ili kukabiliana na hujuma hiyo na kulinda dini ya Mwenyezi Mungu. Taarifa ya kituo hicho cha Kiislamu imesisitiza kwamba Waislamu wanapasa kusimama imara na kupinga tukio chungu la uchomaji moto Qur'ani Tukufu na pia kuonyesha radiamali kali dhidi ya hatua za kuyahudisha Quds Tukufu katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina. Imesema Waislamu hawapasi kuruhusu Wazayuni kutumia vibaya matukio yanayoendelea sasa katika ulimwengu wa Kiislamu kwa ajili ya kufikia malengo yao haramu duniani. Mwaka 2006 Kituo cha Kiislamu cha Wadhakkir kilianzisha mtandao wa kutoa huduma za intaneti kwa Waislamu na anwani ya mtandao huo ni www.Wathakker.net. 964943
captcha