IQNA

Ayatullah Ali Khamenei:

Izza na heshima ya sasa ya taifa la Iran ni matokeo ya kutekeleza mafundisho ya Qur'ani

0:26 - June 25, 2012
Habari ID: 2353544
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei mapema leo (Jumapili) ameonana na maustadh, maqarii na mahafidh bingwa walioshiriki kwenye Mashindano ya 29 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu yaliyomalizika mjini Tehran juzi Ijumaa.
Hafla hiyo iliyojaa nuru ya Qur'ani Tukufu imefanyika kwa mnasaba wa maadhimisho ya siku ya kuzaliwa Abul Fadhlil Abbas AS, katika Haram ya Imam Ridha AS mjini Mash-had, kaskazini mashariki mwa Iran. Hadhirina wamepata fursa ya kusikiliza usomaji wa kuvutia wa Qur'ani Tukufu kutoka kwa maqarii na mahafidh bora walioshiriki kwenye mashindano hayo.
Ayatullah Khamenei amesema mbele ya hadhirina wa hafla hiyo kwamba kuzingatia aya za Mwenyezi Mungu, kufahamu vizuri maarifa ya Qur'ani pamoja na kuyadiriki na kuyazingatia vizuri mafunzo ya ujumbe uliomo kwenye aya za Qur'ani Tukufu, ni jambo linalohitajika sana hivi sasa katika ulimwengu wa Kiislamu.
Aidha amesisitiza kuwa: Kusoma Qur'ani kwa sauti nzuri na ya kuvutia silo lengo kuu la mafundisho ya Qur'ani Tukufu, bali jambo hilo ni utangulizi wa lazima kwa ajili ya kuzifanya nyoyo zipate unyenyekevu na kuziandaa kwa ajili ya kuelewa na kufahamu inavyopasa mafundisho ya Qur'ani Tukufu na kuyazingatia.
Aidha ameyataja mapenzi makubwa waliyo nayo wananchi wa Iran kwa Qur'ani Tukufu kuwa ni hidaya ya Mwenyezi Mungu kwa taifa hili na inabidi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema Zake hizo.
Ameongeza kuwa: Taifa la Iran linaona fakhari na linajivunia kuona kuwa linapeperusha juu bendera ya utawala wa Qur'ani na Uislamu katika dunia hii ya kimaada na kwamba kwa kutumia subira, istikama na uvumilivu mkubwa, linazidi kuifanya bendera hii ipepee kwa ufakhari mkubwa siku baada ya siku, na kwa kutokana na kuwa macho, kujiimarisha kiuwezo na maendeleo yasiyosita, taifa hili limekuwa mara zote likizishinda njama mbali mbali zinazofanywa na maadui.
Vile vile ameitaja heshima ya Kiislamu liliyo nayo hivi sasa taifa la Iran kuwa ni miongoni mwa matunda ya kutekeleza kivitendo mafundisho bora ya Qur'ani Tukufu na kuongeza kwamba: Mataifa mengine ya Waislamu yanapata funzo kutoka katika kigezo hiki kinachong'ara kwamba, kama taifa fulani litajizatiti kiimani, na kama litakuwa na imani thabiti juu ya ahadi za Mwenyezi Mungu, na kama litasimama kidete na kuwa na istikama katika njia ya Qur'ani na Uislamu, na kama halitadanganywa na tabasamu bandia za maadui, basi litaweza kuzishinda nguvu za zana za kali na za kisasa kabisa na kijeshi, na litaweza pia kufelisha njama kubwa na tata mno za kisiasa, kijasusi na kiuchumi za maadui.
Ayatullah Khamenei aidha ameashiria mipango na hatua za Marekani na Wazayuni za kukabiliana na harakati za Kiislamu na wananchi wa eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika na kusisitiza kuwa: Maadui wavyonza damu za watu na wasaliti, wanaendelea kukabiliana na harakati za Kiislamu zinazozidi kuwa kubwa za wananchi wa eneo hili lakini iwapo harakati za mataifa hayo zitaendelea katika njia ya Qur'ani, basi bila ya shaka yoyote njama zote za maadui zitashindwa tu.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la kufanyika kwa wingi mkubwa majilisi za kuhifadhi na kusoma Qur'ani Tukufu sambamba na kupanuliwa wigo wa mafundisho na masomo yanayohusiana na Kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu kwamba litaifanya anga nzima ya Iran kuzidi kuwa na sura ya Qur'ani na kuongeza kuwa, licha ya kuwepo mambo mengi ya uharibifu, lakini idadi ya vijana wa Iran ya Kiislamu wanaojipamba kwa umaanawi na dua ni kubwa sana na haiwezi kulinganishwa na idadi ya vijana wa nchi nyinginezo wanaojipamba kwa sifa hiyo, na kwamba hilo nalo ni jambo la kushukuriwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia jinsi taasisi na vyombo vya kimataifa vinavyokiri kwamba, maendeleo ya kielimu ya Iran ni mara 11 zaidi ya wastani wa kimataifa na kuongeza kuwa, taifa hili kwa kutegemea vijana wake waumini, limefanikiwa kupata maendeleo makubwa katika nyuga zote za kielimu, kisiasa na ujenzi wa nchi na kwamba maendeleo hayo yataendelea kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu.
Katika mkutano huo, Hujjatul Islam Walmuslimin Muhammadi, Mwakilishi wa Fakihi Mtawala ambaye pia ni Mkuu wa Taasisi ya Wakfu na Mambo ya Kheri ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa ripoti fupi kuhusu Mashindano ya 29 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu yaliyomalizika juzi Ijumaa mjini Tehran na kusema kuwa: Maqarii na mahafidh 103 wa Qur'ani Tukufu kutoka nchi 68 tofauti duniani wameshiriki kwenye mashindano hayo yaliyosimamiwa na majaji 14.
Hujjatul Islam Walmuslimin Muhammadi vile vile ameashiria mapokezi mazuri sana waliyoyapata wageni walioshiriki kwenye mashindano hayo na kusema kuwa, idadi ya vijana imeongezeka mara hii kati ya maqarii na mahafidh wa Qur'ani Tukufu jambo ambalo amesema linatoa bishara nzuri na kuongeza kuwa, Taasisi ya Wakfu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina mipango maalumu ya miaka minne na kupitia mipango hiyo imekusudia kuandaa na kulea watu milioni moja waliohifadhi Qur'ani na maqarii milioni moja kwa uwezo na taufiki ya Mwenyezi Mungu.

captcha