IQNA

Qarii wa Sierra Leone:

Aya za Qur'ani zinapaswa kuonekana katika maisha ya mahafidhi wa kitabu hicho

21:26 - June 25, 2012
Habari ID: 2354317
Hifdhi ya Qur'ani inapaswa kuambatana na kutafakari katika aya za kitabu hicho na kutumia mafundisho yake kwa kadiri kwamba aya za Qur'ani zionekane katika maisha ya maqarii na mahufadhi wa kitabu hicho.
Hayo yamesemwa na qarii Abdulqadir Jalo kutoka Sierra Leone ambaye alishiriki katika Mashindano ya 29 ya Kimataifa ya Qur'ani yaliyomalizika hivi karibuni mjini Tehran. Ameongeza kuwa lengo lake la kuhifadhi Qur'ani nzima ni kuwa karibu na maneno ya Mwnyezi Mungu na si kushinda katika mashindano ya Qur'ani.
Abdulqadir Jalo amesisitiza kuwa mashindano ya Qur'ani hususan yale ya kimataifa yanayofanyika katika kiwango cha juu yanaweza kuwa changamoto kubwa kwa maqarii ili waweze kupima uwezo na maendeleo yao na kutambua udhaifu na nakisi zao.
Ustadh Jalo amesema kuwa mashindano ya kimataifa ya Qur'ani pia yanawapa fursa washiriki kutambua mbinu mbalimbali za hifdhi ya Qur'ani katika nchi tofauti na kubadilishana uzoefu katika medani hiyo.
Jalo amesema Qur'ani inaunganisha nyoyo za Waislamu na kwamba mashindano ya kimataifa kama ya Tehran yanaimarisha mfungamano na umoja wa kidini na kiroho kati ya Waislamu.
Qarii huyo wa Sierra Leone ambaye aliwahi pia kushiriki katika mashindano ya kimataifa ya Qur'ani ya Saudi Arabia na Morocco amesisitiza kuwa mashindano ya kimataifa ya Qur'ani yanayofanyika nchini Iran ni ya aina yake. 1037442

captcha