Katika mahojiano yake na IQNA, Omar Abdullah Salim kutoka Dar es Salaam Tanzania amesema amewahi kushiriki katika mashindano ya Qur’ani Misri na Senegal na kwa hakika mashindano haya ya Iran ni ya kiwango cha juu sana na yenye nidhamu nzuri.
'Idadi ya nchi zilizoshiriki pia ni kubwa sana,' amesema Salim.
Ameongeza kuwa kwa kuzingatia idadi kubwa ya washiriki mashindano haya yana nafasi kubwa na muhimu katika kuleta Umoja miongoni mwa Waislamu.
Ameongeza kuwa: 'Ni wazi kuwa kuandaliwa mashindano hayo kuna nafasi kubwa katika kuleta Umoja wa Waislamu. Hapa nimeweza kukutana na Waislamu kutoka nchi mbalimbali na kubadilisana nao mawazo kuhusu masuala ya Qur’ani na masuala mengine yanayowashusu Waislamu.' Aidha ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa juhudi zake hizo za kuwaunganisha Waislamu na ametoa wito kwa Waislamu wote kufuata na kutekeleza aya ya Qur’ani isemayo 'Na shikamaneni na Kamba ya Allah na wala msifarakiane.' Sura Aal Imran 103.
Hafidh huyu wa Qur'ani kutoka Tanzania amesema: 'Nimejifunza mengi na natoa wito kwa Waislamu wa Tanzania kufuata mfano wa watu wa Iran ambao wamefanya bidii sana katika harakati za Qur’ani na kulipa umuhimu mkubwa suala la kuhifadhi Qur’ani.'
Mashindano ya 29 ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu Iran yalianza Tehran tarehe 27 Rajab ( 17 Juni) kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kubaathiwa Mtume SAW na kuendelea hadi tarehe mbili Shaaban sawa na 22 Juni. Mashindano hayo yalikuwa na washiriki 100 kutoka nchi 65 za Kiislamu za zisizokuwa za Kiislamu.
1037952