Akiashiria mazungumzo ya hivi karibuni yaliyofanyika nchini Russia sambamba na kushadidishwa kwa mbinyo wa Magharibi dhidi ya wananchi wa Iran, Ayatullah Kazem Sidiqi amesema, taifa la Iran halitetereshwi na vikwazo hasa kwa kuzingatia kuwa Iran tayari imestawi na kwamba, vikwazo ndivyo vinavyoliwezesha taifa hili kusonga mbele.
Akinukuu maneno ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kuhusiana na vikwazo hivyo, Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya Tehran amesema kuwa, vikwazo vya aina yoyote vitakavyowekwa na nchi za Magharibi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, vitakuwa na taathira mbaya kwa uchumi wa nchi zenyewe za Magharibi.
Aidha amelipongeza taifa la Misri kwa kumchagua Muhammad Mursi wa kundi la Kiislamu la Ikhwanul Muslimin, katika uchaguzi wa rais nchini humo na kusema kuwa, ushindi huo unaonyesha wazi jinsi wananchi wa Misri walivyoshikamana na dini tukufu ya Kiislamu.
Amesisitiza kuwa, uchaguzi wa Misri umetoa ujumbe kwa nchi nyengine kuwa, Hosni Mubarak dikteta wa nchi hiyo ameondoka, hivyo madikteta wa nchi nyingine nao wataondoka na kwamba Marekani na nchi nyingine za kibeberu haziwezi kuwalinda madikteta hao, hata kama zitafanya juhudi chungu nzima za kuwakandamiza wananchi.
1040590