Kituo cha PressTv kimeripoti kuwa jarida la Kifaransa la "60 Million Consumers" limechapisha ripoti ya uchunguzi ambao umebaini kuwa makampuni ya Coca Cola na Pepsi Cola yanatumia kileo katika utengenezaji wa vinywaji hivyo, suala ambalo limeifanya Jumuiya ya Waislamu wa Ufaransa itoe taarifa ikitangaza kuwa imeanza kususia bidhaa hizo.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa Taasisi ya Taifa ya Watumiaji (National Consumer Institute (INC)), mada 19 zinazotumiwa katika utengenezaji wa vinywaji vya Coca Cola na Pepsi Cola vimefanyiwa utafiti na kuonesha kuwa kuna kileo cha miligramu 10 katika kila lita moja ya vinywaji hivyo.
Mkuu wa Jumuiya ya Waislamu wa Ufaransa Muhammad Bishari amesema: "Baada ya kushuhudia matokeo ya uchunguzi huo tunahisi kwamba tumehadaiwa. Makampuni makubwa yanaelewa kwamba Waislamu wanatumia vinywaji vya Pepsi na Coca Cola na hatua ya kutoandikwa kiwango cha alkoholi kilichomo ndani ya vinywaji hivyo ni sawa na kuwahadaa Waislamu."
Amezilaumu pia taasisi nyingine za Kiislamu nchini Ufaransa kwa kunyazia kimya kitendo hicho na kusema taasisi muhimu za Kiislamu zinapaswa kutekeleza majukumu yao katika suala hilo. 1040907