IQNA

16:54 - July 07, 2012
Habari ID: 2362711

Mazungumzo ya Rais Ahmadnejad wa Iran na Rais Mursi wa Misri

Rais wa Misri amesisitiza juu ya udharura wa kufanyika juhudi na kushirikiana Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Misri kwa ajili ya kudhamini maslahi ya mataifa hayo mawili na kufikia malengo yao ya pamoja.

Rais Muhammad Mursi wa Misri amesema hayo katika mazungumzo yake ya simu na Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Iran na kuongeza kuwa nchi hizo mbili zitaendelea kupiga hatua kuelekea kwenye malengo na matarajio ya mataifa yao.
Mursi amesema anatarajia kukutana na mwenzake wa Iran katika mkutano ujao wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) mjini Tehran na kusema jumuiya hiyo ni taasisi muhimu inayokusanya pamoja nchi nyingi za Kiislamu na zisizo za Kiislamu duniani.
Rais wa Misri amesifu misaada na uungaji mkono wa Iran kwa taifa la Misri na akamtaka Rais Ahmadinejad kuwasilisha salamu, upendo na urafiki wa watu wa Misri kwa taifa la Iran na kiongozi wake mkuu Ayatullah Ali Khamenei.
Kwa upande wake Rais Ahmadinejad ameashiria masuala mengi ya kihistoria na kiutamaduni yanayoyakutanisha pamoja mataifa ya nchi hizo mbili na kusisitiza kuwa Wairan siku zote wamekuwa bega kwa bega na taifa la Misri.
Rais Ahmadinejad amesema, kwa kutegemea sheria aali na zilizoendelea za Uislamu, Waislamu wanaweza kudhihirisha mfano wa jamii bora kwa walimwengu. Vilevile amemwalika Rais wa Misri kushiriki katika mkutano wa jumuiya ya NAM utakaofanyika mwezi Agosti mwaka huu mjini Tehran.
1045881
captcha