Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, Khalid Aliyu Abubakar, Katibu Mkuu wa Jama'atu Nasril Islam (JNI) amesema: 'Ni jambo la kawaida kwa uongozi wa JNI kufanya mikakati kabambe ya kujiandaa kwa ajili ya kuukaribisha Mwezi wa Ramadhani ikiwa ni pamoja na kuweka mpango wa kuutafuta mwezi mwandamo.'
Amesema kutafanyika kongamano la Kiislamu litakalowakutanisha pamoja wanazuoni watakaochunguza masuala ya kifiqhi kuhusu suala la mwezi mwandamo katika Uislamu kwa lengo la kuzuia hitilafu zilizoibuka mwaka jana.
Kwa mujibu wa mahesabu ya kifalaki, Mwezi Mtukufu wa Ramadhani utaanza Ijumaa Julai 20; kumekuwepo migongano katika nchi za Kiislamu kutokana na hitilafu zilizoko baina ya maulamaa kuhusu suala hilo.
Kuna kundi la wanazuoni wanaoamini kuwa iwapo mwezi utaonekana katika nchi moja, basi Waislamu walio katika nchi yoyote inayokutana na nchi hiyo katika sehemu ya usiku wanapaswa kufunga. Kundi la pili la wanazuoni ni wale wanaosisitiza kuwa Waislamu kote duniani wanapaswa kufuata kalenda ya Hijria Qamaria inayoainishwa na Saudi Arabia. Kuna kundi la tatu la wanazuoni wanaopinga mitazamo hiyo miwili na kusema suala la kuainisha kuanza au kumalizika Mwezi wa Ramadhani linasimamiwa na uongozi wa Kiislamu katika nchi na hivyo Waislamu katika nchi husika wanapaswa kufuata tangazo la uongozi wao.
1047061