IQNA

Maonyesho ya nuskha za maandishi ya mkono za Qur'ani Tukufu kufanyika Imarati

17:52 - July 24, 2012
Habari ID: 2376362
Maonyesho ya nuskha za Qur'ani Tukufu zilizoandikwa kwa mkono katika karne za kale, yamepangwa kufanyika mjini Dubai tokea tarehe 27 mwezi huu wa Julai kwa ushirikiano wa Kituo cha Utamaduni na Turathi cha Imarati.
Maonyesho hayo yatafanyika katika Kituo cha Utamaduni cha Barajman katika mji uliotajwa.
Kwa mujibu wa gazeti la Imarati la al-Bayan, maonyesho hayo ambayo yamepangwa kuendelea hadi tarehe 16 Agosti ni fursa nzuri kwa watu kushuhudia kwa karibu maandishi ya Qur'ani yaliyoandikwa kwa mkono katika karne zilizopita na maendeleo yaliyofikiwa katika uandishi wake hadi leo. Nuskha hizo ni pamoja na zile zilizoandikwa kwa hati za kale za kufi, mashariki na za Morocco.
Sehemu nyingine ya maonyesho hayo itahusiana na Qur'ani adimu zilizoandikwa miaka 1000 iliyopita na vilevile nuskha za maandishi ya mikono zilizoandikwa kwa lugha za Kifarsi na Kituruki.
Akielezea sababu za kuonyeshwa nuskha hizo katika kipindi kilichotajwa, Sabia Khandawani, mkuu wa kitengo cha mawasiliano ya umma na mauazo cha Kituo cha Barajman amesema kuwa kipindi hicho kimeainishwa kwa ajili ya maonyesho ya Qur'ani Tukufu kwa kutilia maanani kwamba Qur'ani yenyewe iliteremshwa katika mwezi mtukufu wa Ramadhani. Amesema Waislamu na wasio Waislamu wote wataruhusiwa kuyatembelea maonyeho hayo ili kushuhudia kwa karibu nuskha za kihistoria za Qur'ani Tukufu, ambayo ni marejeo muhimu ya Waislamu katika maisha yao ya humu duniani na huko Akhera. 1060263
captcha