Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei alasiri ya leo (Alkhamisi) amekutana na Rais wa Tajikistan na kusema kuwa lugha, utamaduni wenye historia ndefu na wa pamoja wa mataifa ya eneo hili ni uwanja mzuri wa kupanua na kuimarisha uhusiano wa pande mbili na pande kadhaa na kujenga mustakbali bora.
Amekaribisha uhusiano mzuri wa pande hizo katika nyanja mbalimbali na akasema kuheshimiwa ada, itikadi na desturi za wananchi huvutia uungaji mkono wa wao na serikali yoyote inayopata uungaji mkono kama huo inaweza kusimama imara mbele ya chokochoko za kigeni.
Kwa upande wake Rais Imam Ali Rahman wa Tajikistan ameeleza nyanja mbalimbali za ushirikiano wa pande mbili na ametaka kuimarishwa zaidi uhusiano wa Tehran na Doshanbe katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni.
Rais wa Tajikistan ameipongeza Iran kwa maandalizi ya hali ya juu ya mkutano wa viongozi wa Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) na akamwambia Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi kwamba hotuba yake katika ufunguzi wa mkutano muhimu wa viongozi wa NAM itaifanya jumuiya hiyo kuwa na taathira kubwa zaidi.
Bwana Rahman ameashiria baadhi ya njama zinazofanywa na nchi a kigeni kwa ajili ya kuvuruga amani na kuzibakisha nyuma nchi za eneo hili na akasema kuwa nchi hizo zitaendelea kusimama kidete mbele ya njama hizo kwa kusaidiana. 1088182