
Katika taarifa iliyotolewa Alhamisi, harakati hiyo ya Muqawama au mapambano ya Kiislamu ya Lebanon ilielezea kitendo hicho kuwa ni uhalifu wa aibu na tendo ovu lililofanywa na raia wa Kimarekani, kwa mujibu wa ripoti ya Al-Alam.
Taarifa hiyo ilisisitiza kuwa kitendo hicho cha kudharau Qur'ani ni shambulio la wazi dhidi ya vitakatifu vya Waislamu, na pia ni dharau kwa misingi ya maadili ya kidini na kibinadamu ambayo dini zote za mbinguni zinasimamia.
Hezbollah, ikikosoa vikali mwenendo wa serikali ya Marekani, ilibainisha kuwa kukataa kwa Washington kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wahusika wa matusi kama haya, kwa kisingizio cha uongo cha uhuru wa kujieleza na uhuru wa kusema, ni dalili ya kuficha na kulinda makusudi vitendo hivi hatari na vya uchochezi na serikali ya Marekani yenyewe.
Taarifa hiyo iliendelea kusema kuwa uhalifu huu si tukio la mtu mmoja binafsi, bali wahusika wake ni watu wanaotumiwa kama zana na vikaragosi mikononi mwa kiburi cha kimataifa kinacholenga kuidhoofisha Dini Tukufu ya Kiislamu.
Aidha, Hizbullah ilizitaka mataifa ya Kiarabu na Kiislamu, pamoja na wafuasi wa dini zote za mbinguni, kuanzisha kampeni pana ya kulaani kitendo hiki cha kihalifu, na kusimama kidete dhidi ya mashambulizi yoyote yanayolenga vitakatifu na thamani takatifu za Uislamu na dini nyingine za mbinguni.
Wiki iliyopita, katika tukio lenye utata mkubwa mjini Plano, jimbo la Texas, mgombea wa Seneti kutoka chama cha Republican cha Florida, Jake Lang, alilitukana vikali Qur'ani Tukufu kwa kuweka nakala ya Kitabu Kitukufu kinywani mwa nguruwe wakati wa maandamano. Kitendo hicho kiliwaghadhibisha Waislamu, wanaharakati wa haki za binadamu, pamoja na wachunguzi wa kimataifa, na kusababisha mshtuko mkubwa ndani na nje ya Marekani.
Katika video iliyosambazwa kupitia mitandao ya kijamii, Lang alionekana akimbeba mwana-nguruwe huku Qur'ani ikiwa kinywani mwake, akimtaja mnyama huyo kuwa ni “udhaifu wa Uislamu,” na kusema: “Huu ndio udhaifu wenu, Waislamu. Tutawarudisha mlipotoka, tukiwa tumebeba nguruwe mikononi na Kristo mioyoni mwetu.”
3495783