
Ahmed Fouad Heno, Waziri wa Utamaduni wa Misri, alizindua rasmi makumbusho hayo Jumatatu, huku Waziri wa Awqaf, Osama Al-Azhari, pia akihudhuria hafla ya ufunguzi.
Makumbusho haya yanasherehekea urithi wa kiroho na kiutamaduni wa Misri na kuheshimu sauti mashuhuri za usomaji wa Qur’an Tukufu.
Ndani yake kuna kazi binafsi na vitu vya waqari wakubwa 11 wa Misri, akiwemo Muhammad Rifa’at, Abdul Fattah Shasha’ei, Taha Al-Fashni, Mustafa Ismail, Mahmoud Khalil Al-Husari, Muhammad Siddiq Minshawi, Abu al-Ainain Shuaisha, Mahmoud Ali Al-Banna, Abdul Basit Abdul Samad, Muhammad Mahmoud Tablawi, na Ahmed Al-Ruzifi.
Sehemu moja imeonesha mkusanyiko wa vitu binafsi vya Abdul Basit pamoja na bango linaloeleza wasifu na huduma zake za Qur’an kama qari maarufu wa Misri na ulimwengu wa Kiislamu.
Miongoni mwa vitu vilivyowekwa hadharani ni picha ya Abdul Basit akiwa na watoto wake, gramofoni, kilemba, tasbihi kadhaa, kofia, vyetu vya heshima, na sanduku lenye nakala ya Qur’an Tukufu.
Alaa Husni, mjukuu wa Mustafa Ismail, aliambia gazeti la Misri Al-Youm kuwa familia ya marehemu qari huyo imechangia baadhi ya vitu binafsi vya babu yake katika makumbusho, ikiwemo tasbihi, fimbo, saa, kilemba, nguo, redio na bango lenye vipande vya magazeti vinavyoonesha alivyoenziwa na Rais Gamal Abdel Nasser wa wakati huo, na uwepo wake pamoja na Rais wa zamani Muhammad Anwar Sadat katika ziara ya al-Quds.
Biransa, binti ya Sheikh Muhammad Mahmoud Tablawi, alisema wizara ya Awqaf ilizungumza na familia ya qari huyo mwaka mmoja uliopita kukusanya vitu vyake, na familia ilikuwa na hamu ya kuchangia Qur’an yake, nguo na picha binafsi katika makumbusho.
“Uzinduzi wa makumbusho haya ni ishara nzuri sana na umeleta pamoja kumbukumbu za waqari mashuhuri wa Qur’an ambao hawatapatikana tena,” aliongeza.
3495784