IQNA

Wayamani walaani kuvunjiwa heshima Qur’ani Tukufu Marekani

15:28 - December 19, 2025
Habari ID: 3481683
IQNA – Mashirika na taasisi mbalimbali za Kiyemeni yamelaani kitendo cha hivi karibuni cha kudhalilisha Qur’an Tukufu nchini Marekani, na yameunga mkono mwito wa kiongozi wa Ansarullah (Houthi) wa kufanya maandamano ya kulaani kitendo hicho cha kufuru.

Wiki iliyopita, katika tukio lenye utata lililofanyika Plano, jimbo la Texas, mgombea wa Seneti wa chama cha Republican kutoka Florida, Jake Lang, alivunjia heshima Qur’an Tukufu kwa kuiweka katika kinywa cha nguruwe wakati wa maandamano. Kitendo hicho kilizua hasira kubwa miongoni mwa Waislamu, wanaharakati wa haki za binadamu, na wadau wa kimataifa, na kusababisha mshtuko mpana ndani na nje ya Marekani.

Katika video iliyosambazwa mitandaoni, Lang alionekana akibeba nguruwe mdogo huku akisema maneno ya dharau, akidai kuwa Qur’an ni “udhaifu wa Uislamu” na akatamka: “Hii ndiyo udhaifu wenu, Waislamu. Tutawarudisha mlipotoka, tukibeba nguruwe mikononi na Kristo mioyoni mwetu.”

Serikali ya Mabadiliko na Ujenzi ya Yemen, katika tamko lake, ilisisitiza kuwa kukabiliana na matusi haya ya makusudi na ya mara kwa mara ni wajibu wa kidini kwa Waislamu wote duniani. Tamko hilo liliwataka wananchi wa Yemen na taasisi zote za kitaifa kujibu mwito wa kiongozi wa Ansarullah kwa uwajibikaji na kwa uelewa, kuchukua hatua na kutangaza msimamo dhidi ya matusi ya mara kwa mara kwa sehemu takatifu na ukiukaji wa heshima ya Msikiti wa Al-Aqsa unaofanywa na Wazayuni, na kushiriki katika maandamano makubwa ya Ijumaa.

Baraza Kuu la Mahakama ya Yemen pia lilialika mataifa ya Kiarabu na Kiislamu, wanazuoni na mashirika ya kimataifa husika kukabiliana na mashambulizi haya dhidi ya utakatifu wa Kiislamu. Katika tamko lake, baraza hilo lilikemea udhalilishaji wa Qur’an Marekani na kusisitiza kuwa lengo la mashambulizi haya ni kuchochea chuki, na kwamba hayana uhusiano wowote na uhuru wa kujieleza.

Baraza hilo liliitaka dunia kukomesha vitendo hivi vya kibaguzi dhidi ya Uislamu na Qur’an Tukufu, na likaunga mkono mwito wa kiongozi wa Ansarullah wa kuchukua hatua za wananchi kupinga udhalilishaji wa Qur’an.

Chama cha Wanazuoni wa Yemen, kwa upande wake, kilisema kuwa uhalifu huu unaonesha chuki ya kina na uadui wa wazi dhidi ya kila kinachowakilisha heshima na hadhi ya Ummah wa Kiislamu. Tamko lao lilionyesha kuwa adui ameielekeza mishale yake ya kisasi kwa Qur’an Tukufu, kwa sababu anajua kuwa Qur’an ndiyo chanzo cha nguvu, maendeleo na umoja wa Ummah.

Chama hicho kiliwataka Waislamu wote kulaani uhalifu huu na kutangaza upinzani wao dhidi yake, na kiliwaalika wanazuoni, wahubiri na wasomi wa Ummah kutimiza wajibu wao wa kidini na kimaadili wa kuelimisha mataifa, kupambana na maadui wa Ummah wa Kiislamu, na kupinga miradi yao ya uhasama.

Taarifa ya Kiongozi wa Ansarullah

Kiongozi wa harakati ya Muqawama ya Ansarullah nchini Yemen amelaani vikali kitendo cha hivi karibuni cha kuvunjia heshima Qur’ani Tukufu kilichofanywa na mwanasiasa wa Marekani huku akiwataka Waislamu kote duniani kusimama imara kulinda matukufu yao.

Katika taarifa yake ya Jumanne, Abdul‑Malik al‑Houthi alikitaja kitendo hicho kuwa ni “jinai dhidi ya matukufu makubwa zaidi ya dini duniani,” akisisitiza kuwa ni sehemu ya “vita vinavyoendelea” dhidi ya Uislamu vinavyoongozwa na Marekani, Uingereza, utawala wa Israel na washirika wao Mashariki na Magharibi.

Leader of Yemen’s Ansarullah resistance movement Abdul-Malik al-HouthiKwa mujibu kiongozi wa Ansarullah, tawala hizo zinalenga kuharibu jamii za kibinadamu na kuzikoloni. Aliongeza kuwa udhalilishaji wa matukufu ya dini unaenda sambamba na “harakati pana” za kuyafanya mataifa kuwa mateka, kupora rasilimali zao na kuvamia ardhi zao.

Al Houthi amesema mfululizo wa matusi dhidi ya Uislamu, pamoja na vita laini na ngumu vinavyoendeshwa na Uzayuni na washirika wake, ni ishara ya uadui wa wazi dhidi ya Uislamu na Waislamu.

Aidha, amebainisha kuwa vitendo hivyo vinakusudia kudhoofisha nafasi ya Qur’ani Tukufu katika nyoyo za Waislamu na kuwafanya watengane na mafundisho yake, jambo linaloonyesha “chuki ya kina” dhidi ya Uislamu.

Akirejea uhalifu wa Israel dhidi ya Wapalestina na maeneo matakatifu ya Kiislamu katika ardhi inayokaliwa kwa mabavu, Al Houthi amesisitiza kuwa matendo hayo, pamoja na uungaji mkono wa Magharibi kwa Israel, ni uthibitisho zaidi wa uadui huo.

Amesisitiza kuwa Waislamu—serikali na wananchi, wasomi na umma kwa ujumla, wana wajibu wa kidini na kimaadili kukabiliana na nguvu za dhulma na upotoshaji zinazoongozwa na Uzayuni.

Al Houthi ameonya kuwa kutojali na kunyamaza mbele ya matusi kama haya kunawatia nguvu maadui na kunawakilisha udhaifu mkubwa wa imani, maadili na misingi ya kiroho.

Pia alikosoa ukosefu wa msimamo madhubuti wa kisiasa na kiuchumi au  kutoka ulimwengu wa Kiislamu licha ya kuwa na idadi ya Waislamu takribani bilioni mbili, akisema kuwa msimamo wa wasomi na mataifa ya Waislamu kwa kiasi kikubwa umeakisi ule wa serikali zao.

Kiongozi huyo wa Ansarullah amewataka wananchi wa Yemen kufanya maandamano makubwa Ijumaa hii kulinda utukufu wa Qur’ani Tukufu na maeneo matakatifu ya Kiislamu, wakiendeleza maandamano ya kila wiki ya kuunga mkono wananchi wa Palestina.

Habari zinazohusiana
captcha