IQNA

Uwanja wa Bibi Zahra (SA) katika Haram ya Imam Ali (AS), upanuzi mkubwa zaidi wa eneo takatifu la Kiislamu

15:09 - December 19, 2025
Habari ID: 3481681
IQNA – Eneo  mpya katika Haram Tukufu ya Imam Ali (AS) mjini Najaf, ambalo linatambuliwa  kwa ukubwa wake wa kipekee na sifa bainifu za usanifu wa Kiislamu, umezinduliwa rasmi Jumanne huko Najaf, Iraq.

Baada ya miaka 14 ya ushiriki wa umma na juhudi za wapenzi na wafuasi wa Ahl al-Bayt (AS), ujenzi wa Uwanja wa Bibi Fatima Zahra (SA), uliopo karibu na Haram ya Imam Ali (AS), umekamilika na kukabidhiwa rasmi kwa wasimamizi wa haram hiyo mjini Najaf, Iraq.

Hafla ya uzinduzi ilifanyika Jumatano, ikihudhuriwa na viongozi waandamizi wa Iran na Iraq. Mradi huu umeelezwa kwa mapana kuwa ni zawadi kutoka kwa wapenzi wa Bibi Fatima Zahra (SA) kwa haram ya mume wake mtukufu, Imam Ali (AS), Imam wa kwanza wa Waislamu wa madhehebu ya Shia.

Hadi mwanzoni mwa miaka ya 2010, Haram ya Imam Ali (AS) ilikuwa na eneo dogo kiasi, ikijumuisha zaidi chumba cha dhariha tukufu na vyumba vichache vilivyoambatana nacho. Baada ya kuporomoka kwa utawala wa Saddam na kuongezeka kwa fursa za wafanyaziara kufika Najaf, hasa kufuatia kupanuka kwa hija ya Arbaeen duniani, haja ya kupanua haram ikawa dharura kubwa.

Kutokana na hali hiyo, uongozi wa haram ulianzisha mpango mkubwa wa upanuzi. Hatua ya kwanza na kubwa zaidi ilikuwa ni ujenzi wa Uwanja wa Bibi Zahra (SA), jengo kubwa lililojengwa upande wa magharibi wa haram. Mradi huu ulianza mwaka 2011 katika eneo lenye urefu wa takriban mita 400 na upana wa mita 150, huku jumla ya eneo lililojengwa likifikia takriban mita za mraba 220,000.

Makao Makuu ya Iran ya Ukarabati na Maendeleo ya Maeneo Matukufu ya Kiislamu yalisimamia mradi huu. Kwa mujibu wa maafisa, huu ni mradi wa tatu kwa ukubwa katika historia ya upanuzi wa maeneo ya kidini katika ulimwengu wa Kiislamu, baada ya upanuzi wa Msikiti Mkuu wa Makka na Msikiti wa Mtume (SAW) mjini Madina.

Mfumo maalumu wa michango ya umma uliwezesha Waislamu wa Kishia na wapenzi wa Ahl al-Bayt (AS) kutoka pande zote za dunia kushiriki kwa kuchangia kifedha.

Licha ya kusitishwa kwa muda mfupi wakati wa janga la COVID-19, ujenzi uliendelea kwa uthabiti. Katika kipindi cha miaka 14 iliyopita, sehemu kadhaa za ibada ndani ya ua huo zilifunguliwa hatua kwa hatua kwa wafanyaziara. Hafla ya Jumanne iliashiria kukamilika rasmi kwa mradi mzima na kukabidhiwa kikamilifu kwa uongozi wa Haram ya Imam Ali (AS).

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wakuu wa kidini na kisiasa, akiwemo Hujjatul-Islam Mohammad Mohammadi Golpayegani, mkuu wa ofisi ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu; maafisa wa Haram ya Imam Ali (AS); Seyed Mehdi Khamoushi, mkuu wa Shirika la Wakfu na Misaada la Iran; na Hassan Palarak, naibu mkuu wa bodi ya wadhamini wa makao makuu ya ukarabati wa haram, pamoja na maafisa wengi wa Iran na Iraq.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mohammadi Golpayegani aliwasifu wahandisi na wasanii waliotekeleza mradi huo, akisema ua huo unaakisi “mapenzi na ikhlasi ya watu wa Iran, Iraq na mataifa mengine kwa Ahl al-Bayt (AS).”

Kwa upande wake, Hassan Palarak aliwaambia waandishi wa habari pembezoni mwa uzinduzi huo: “Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwapa watu wa Iran fursa ya kuanzisha eneo linaloitwa kwa jina la Bibi Fatima Zahra (SA) karibu na Haram ya mume wake mtukufu. Uwanja huu umekamilika kwa juhudi za dhati na ikhlasi ya watu.”

Aliongeza kusema: “Hata sehemu elfu moja ya kazi iliyofanywa hapa haiwezi kunaswa na kamera yoyote.” Palarak alisema ua huo, wenye eneo la takriban mita za mraba 230,000, ulikamilishwa ndani ya chini ya miaka mitano ya kazi nzito, kwa kutumia usanifu wa Kiislamu na michango ya wasanii wengi kutoka ulimwengu wa Kiislamu.

 

Pia alitaja miradi mingine inayoendelea, ikiwemo upanuzi wa Haram ya Imam Hussein (AS) mjini Karbala, ambako kunapangwa kujengwa nyua nne mpya.

Kuhusu Uwanja wa Bibi Zahra (SA)

Uwanja wa Bibi Zahra ni miongoni mwa miradi mikubwa na ya kina zaidi ya upanuzi katika historia ya haram tukufu za Kishia. Umebuniwa kukidhi kikamilifu mahitaji ya kidini, kitamaduni na huduma za Haram ya Imam Ali (AS), na umegawanywa katika sehemu mbili kuu: eneo la ibada (ziyarah) na eneo lisilo la ibada.

Miongoni mwa sifa zake za kipekee ni ujenzi wa muqarnas kubwa zaidi kuwahi kujengwa katika eneo la Kiislamu—aina ya mapambo ya usanifu wa dari yenye maumbo tata na ya kuvutia.

Mradi huu pia una kazi pana za plasta, mapambo ya dari ya mtindo wa Yazd, maandishi ya kaligrafia yenye aya za Qur'ani Tukufu na dua, pamoja na vigae vya nje vilivyopambwa kwa sanaa ya mosaiki. Kwa mujibu wa maafisa, eneo hilo ni makumbusho ya kudumu ya sanaa ya usanifu wa Kiirani-Kiislamu.

Sehemu ya ibada ina ukubwa wa mita za mraba 29,000, ikijumuisha ghorofa kuu nne na mezzanine tatu, zenye jumla ya eneo la takriban mita za mraba 85,000. Ina uwezo wa kupokea hadi wafanyaziyara 100,000 kwa saa moja. Huduma zake ni pamoja na kumbi za swala katika ngazi tatu, uwanja wa wazi, vyumba vya kielimu (hawza), vituo vya afya, miundombinu ya kiufundi, maghala, vyoo, na huduma nyingine za wafanyaziyara.

.

Ndani ya kumbi za swala, kuna nguzo zaidi ya 1,200 zilizopambwa kwa mawe, kila ghorofa ikiwa na aina tofauti ya jiwe. Zaidi ya kuba 800 za ndani zimejengwa katika kumbi hizo, zikionyesha ukubwa na fahari ya usanifu wa Kiislamu wa Kiirani.

Sehemu isiyo ya ibada inajumuisha makumbusho, maktaba, majengo ya utawala, nyumba ya wageni na ukumbi wa mapokezi ya jadi (mudhif), mgahawa, maeneo ya kutawadha na vyoo, pamoja na eneo maalumu la maegesho. Maeneo haya yamelenga kutoa huduma za kitamaduni, kijamii na kiuhudumiaji kwa wafanyaziara.

Maktaba ya ghorofa sita, iliyojengwa katika eneo la mita za mraba 3,100, ina uwezo wa kuhifadhi zaidi ya vitabu 250,000. Nyumba ya wageni na huduma za mapishi zinaweza kuandaa hadi milo 10,000 kwa mlo mmoja.

Huduma za vyoo zina vitengo 900, ambavyo vikijumlishwa na vilivyokuwepo awali karibu na haram, vina uwezo wa kuhudumia zaidi ya wafanyaziara 140,000. Makumbusho yenyewe yana ghorofa sita na jumla ya eneo la mita za mraba 18,000.

Kwa kukamilika kwa Uwanja wa Fatima Zahra (SA), Haram ya Imam Ali (AS) sasa ina maeneo ya kisasa ya ibada yaliyochochewa na usanifu wa kale wa Kiirani-Kiislamu—maeneo ambayo wafanyaziara wengi kutoka Iran na mataifa mengine tayari wameyashuhudia wakati wa matembezi ya Arbaeen na ziara zao Najaf.

3495776

captcha