IQNA

Imam Khamenei Aonana na Watu Wanaojitolea katika Masuala ya Afya Nchini

13:58 - January 01, 2013
Habari ID: 2473912
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Jumatatu ameonana na majimui ya watu wanaojitolea katika masuala ya afya nchini Iran na kusema kuwa suala la "usalama wa kiafya, tiba na utabibu" ni moja ya masuala ya kimsingi kabisa na ya daraja la kwanza nchini Iran
Aidha amepongeza kazi zinazofanywa na wananchi katika uwanja huo amesema kuwa, kila mahala ambapo imani, uwezo na nia ya wananchi inapokuwa kwenye medani, huweza kufanikisha utekelezaji wa kazi nyingi kwa baraka kubwa sana na huweza kutatuwa matatizo yaliyopo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia nafasi muhimu ya wananchi katika nyuga zote muhimu iwe za kisiasa, au kiuchumi, au kiafya, au kutamaduni, au elimu na malezi na kusisitiza kuwa, asili ya Mapinduzi ya Kiislamu nayo imeegemea kwenye uwepo huo makini wa wananchi na lau kama wananchi wasingelijitokeza vilivyo katika medani, basi wanasiasa na mirengo ya kisiasa isingeliweza kufanya chochote.
Amesisitizia pia wajibu wa kupewa kipaumbele suala la usalama wa kiafya, tiba na utabibu katika masuala mengi nchini na kuongeza kwamba: Viongozi wenye uchungu na nchi wanapaswa kuweka mikakati mizuri kwa namna ambayo masuala yote yaweze kufuatiliwa vizuri kiutendaji ili wananchi wasiwe na wasi wasi hata kidogo katika suala la usalama wa afya zao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kulindwa muundo wa hivi sasa wa jumuiya na taasisi za kujitolea katika mambo ya kheri - yaani muundo wake wa kuendeshwa na wananchi - kuwa ni jambo muhimu sana na kuongeza kwamba, haipasi kuruhusu muundo uliojifunga wa kiidara na ambao umezoeleka sana, uharibu asili na usafi wa harakati za watu katika jumuiya za wananchi.
Katika sehemu ya mwisho ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kivutio kikubwa zaidi cha watu wanaojitolea katika mambo ya kheri ni kuzaa matunda juhudi zao na kuonekana wazi athari za kazi zao.
Amefafanua zaidi akisema: Kazi za namna hiyo za kujitolea katika mambo ya kheri huenda sambamba na radhi za Mwenyezi Mungu Mtukufu na kwamba kazi yoyote ya kheri ina nafasi muhimu mbele ya Mwenyezi Mungu na haipiti bure.
Mwanzoni mwa mkutano huo, Sayyid Reza Niri, Katibu wa Baraza la Watu Wanaojitolea katika Masuala ya Afya ya Iran amezungumzia kwa ufupi kazi, muundo, huduma, mipango, mahitaji na ratiba za baraza hilo na kuongeza kwamba, msingi wa kuundwa na namna ya ufanyaji kazi wa baraza hilo katika kipindi chote hiki cha miaka mitatu ya tangu kuasisiwa kwake ni miongozo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, aliyetaka kutumiwa vizuri uwezo wa wananchi katika masuala ya usalama wa kiafya nchini.
1164065
captcha