IQNA

10:12 - May 26, 2013
Habari ID: 2538667
Dkt. Husseini katika Siku ya Afrika Tehran

Iran iko tayari kustawisha uhusiano na nchi za Afrika

Waziri wa Utamaduni na Muongozo wa Kiislamu nchini Iran amesema Tehran iiko tayari kuimarisha uhusiano wake na nchi za Afrika.

Seyyed Mohammad Husseini aliyasema hayo Jumamosi jioni mjini Tehran katika hafla ya Siku ya Afrika ambayo huadhimishwa 25 Mei na ambayo imesadifiana na kuwadia mwaka wa 50 tokea kuanzishwa Jumuiya ya Nchi Huru za Afrika OAU iliyobadilisha muundo wake na kuwa Umoja wa Afrika. Akiashiria uzoefu wake wakati akiwa mkuu wa Idara ya Utamaduni katika Ubalozi wa Iran nchini Kenya pamoja na safari zake katika nchi kadhaa za Afrika amesema, baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu Hayati Imam Khomeini alisisitiza kuhusu kustawisha uhusiano na nchi za Afrika. Aidha ameashiria historia ndefu ya ukoloni wa madola ya nchi za Magharibi barani Afrika na kusema hicho ndicho chanzo cha matatizo mengi ya bara hilo. Ameonya kuwa nchi za Magharibi bado zinajaribu kuzikoloni tena nchi za Afrika. Aidha ameelezea matumaini yake kuwa ustawishaji uhusiano wa Iran na Afrika utapelekea kuboreka hali ya bara hilo.

Kikao hicho pia kilihutubiwa na Dkt. Bagher Khoramshad Mkuu wa Shirika la Utamaduni na Mahusiano ya Kiislamu ICRO ambaye amesema Iran iko tayari kushirikiana kikamilifu na nchi za Afrika katika uga wa elimu. Katibu wa kikao hicho Dkt. Dehshiri amesema Iran ina azma ya kushirikiana na nchi za Kiafrika katika uga wa utafiti. Wengine waliohutubia kikao hicho ni mabalozi wa Mali, Uganda na Sierra Leone.

Sherehe hizo za Siku ya Afrika hapa mjini Tehran ambazo ziliandaliwa na Shirika la Utamaduni na Mahusiano ya Kiislamu pia zimehudhuriwa na mabalozi wa nchi za Afrika, Waafrika waishio Iran pamoja na wahadhiri wa vyuo vikuu.
1233583
captcha