IQNA

Mawaziri wa Habari wa nchi za Kiislamu wakutana Tehran

0:42 - December 04, 2014
Habari ID: 2615009
Mkutano wa 10 wa Mawaziri wa Habari wa nchi za Kiislamu (ICIM) umefanyika Jumatano hapa mjini Tehran kwa kuhudhuriwa na Is’haq Jahangiri Makamu wa Kwanza wa Rais na Katibu Mkuu wa OIC.

Kikao hicho cha siku mbili kinahudhuriwa na wawakilishi kutoka zaidi ya nchi 40 kati ya nchi 57 wanachama wa OIC. Akthari ya nchi za Ghuba ya Uajemi ikiwemo Saudi Arabia, Qatar, Kuwait na Imarati zinashiriki katika kikao hicho kinachotarajiwa kumalizika leo. Ushirikiano na kuchukuliwa hatua za pamoja za kihabari katika nchi za Kiislamu kwa ajili ya kukabiliana na misimamo ya kufurutu ada ndio ajenda kuu ya mazungumzo ya Mawaziri wa Habari wa nchi za Kiislamu katika kikao chao cha Tehran.
Akizungumza katika kikao cha ufunguzi hapo jana, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran alisema kuwa, ugaidi na misimamo ya kufurutu ada ndiyo changamoto kubwa zaidi zinazoukabili ulimwengu wa Kiislamu na kwamba, vitendo vya utumiaji mabavu vya kundi la kigaidi la Daesh dhidi ya Waislamu wa Kishia na Kisuni na vilevile wafuasi wa dini nyingine vimezijeruhi mno nyoyo za wanadamu. Is’haq Jahangiri ameashiria njama pana na za kila namna za baadhi ya vyombo vya habari vya Magharibi zenye lengo la kusukuma kadiri iwezekanavyo gurudumu la mpango wa kuuonesha Uislamu kuwa ni tishio na akabainisha kuwa, vitendo vya kinyama vya makundi ya kigaidi vinavyofanyika kwa jina la Uislamu vimekuwa vikienezwa na kutumiwa vibaya na vyombo hivyo vya habari katika fremu ya kutilia nguvu njama za kuuonesha Uislamu kuwa ni tishio. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran amesisitiza kuwa, ni jukumu la Waislamu kufanya hima kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, kunakuweko ulimwengu ambao ndani yake hakuna vitendo vya utumiaji mabavu.
Kwa upande wake Iyad Amin Madani, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) amesema katika sherehe ya ufunguzi wa mkutano huo kwamba, ulimwengu wa Kiislamu unapaswa kukabiliana vikali na aidiolojia ya mielekeo ya kuchupa mipaka. Madani amesisitiza kuwa, Umma wa Kiislamu unakabiliwa na changamoto muhimu ambazo zinatishia amani na utambulisho wa Kiislamu. Katibu Mkuu wa OIC amevikosoa vikali baadhi ya vyombo vya habari vya nchi za Kiislamu ambavyo vinasaidia kueneza fikra za kufurutu ada na kusisitiza kwamba, nchi wanachama wa OIC hazipaswi kuunga mkono fikra za kufurutu ada.
Kwa upande wake, Waziri wa Utamaduni na Muongozo wa Kiislamu wa Iran Ali Jannati amesema kuwa, kufanyika kikao cha Mawaziri wa Habari wa nchi za Kiislamu mjini Tehran ni fursa muhimu kwa ajili ya kuwa na mitazamo ya pamoja kwa shabaha ya kuimarisha amani na utulivu katika ulimwengu wa Kiislamu. Jannati amevitaka vyombo vya habari vya ulimwengu wa Kiislamu kuwaonesha walimwengu sura halisi ya Uislamu.
Siku mbili zilizopita, kulifanyika pia kikao cha wataalamu wa vyombo vya habari wa nchi za Kiislamu ambapo washiriki walionesha kusikitishwa kwao na udhaifu wa vyombo vya habari vya Kiislamu na wakasisitiza juu ya udharura wa vyombo hivyo kuwa na utendaji wenye taathira. Hapana shaka kuwa, kufanyika mkutano wa Mawaziri wa Habari wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu katika kipindi hiki kuna umuhimu mkubwa hasa kwa kutilia maanani matukio yanayojiri hivi sasa katika ulimwengu wa Kiislamu. Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndiyo maana washiriki wakatilia mkazo katika siku ya kwanza ya mkutano wao juu ya kuweko mtazamo mmoja katika ulimwengu wa Kiislamu kwa shabaha ya kukabiliana na fikra za kufurutu ada.../mh

2614997

captcha