Abubakr Shekau ameyasema hayo kupitia ujumbe wa video uliowekwa katika mtandao wa kijamii wa Twitter. Kusambaa habari ya muungano wa makundi hayo ya kitakfiri ambayo ni maarufu kwa kutenda jinai dhidi ya binaadamu, kunathibitisha mahusiano yaliyopo kati ya Boko Haram na Daesh.
Katika siku za awali za mwezi wa Ramadhani mwaka uliopita, kundi la Daesh lilitangaza mipaka ya utawala wa kile ulichokisema kuwa ni khilafa katika nchi za Syria na Iraq. Kuhusiana na suala hilo, katika ripoti iliyotolewa kwa njia ya sauti na kutumwa katika mitandao ya kijamii, msemaji wa kundi hilo la Daesh alimtaja Abubakar al-Baghdadi kuwa khalifa wa kwanza wa dola hilo. Hii ni katika hali ambayo mwezi Agosti mwaka jana, kiongozi wa kundi la Boko Haram pia alitangaza utawala wa khilafa katika maeneo yaliyokuwa yakidhibitiwa na kundi hilo huko kaskazini mwa Nigeria.
Weledi wa mambo waliitaja hatua ya kundi hilo kuwa ni aina fulani ya kufuata nyayo za magaidi wa Daesh na kuthibitisha kuwepo umoja wa kiistratijia kati ya makundi hayo yanayojiona bora duniani. Hivi sasa kundi la Boko Haram lingali linadhibiti maeneo kadhaa ya jimbo la Borno la kaskazini mashariki mwa Nigeria. Kwa mujibu wa weledi wa mambo, muundo wa makundi ya kigaidi barani Afrika uko kwa namna tata na usioeleweka. Swali la msingi ni kwamba, makundi hayo yanapata kwa njia gani fedha za kujiendesha na ni watu gani wanaonufaika na harakati za makundi hayo ya kitakfiri? Ushahidi uliopo unaonesha kuwa, kabla ya jambo lolote, jeshi la Nigeria ambalo lina muundo wa jeshi la Uingereza ndilo linalohusika katika utoaji mafunzo kwa wanachama wa kundi la Boko Haram. Kwa mujibu wa ushahidi huo, askari wa Nigeria walitoa mafunzo kwa kundi hilo katika kambi za siri za nchini humo huku weledi wa mambo wakithibisha pia kwamba Waingereza walitoa mafunzo kwa wanachama wa kundi la kigaidi la ash-Shabab la nchini Somalia. Suala la kuzingatia hapa ni kwamba, msingi wa fikra wa makundi ya kigaidi kama vile Boko Haram, ash-Shabab, Answaru Sharia na mengineyo, unategemea mafundisho ya Kiwahabi na kwa kuegemea fikra za Saudi Arabia. Tangu awali Saudia na Qatar zilieneza fikra za Kiwahabi katika nchi za Kiafrika kupitia kujenga misikiti na shule. Baada ya kutoa mafunzo hayo ya Kiwahabi, nchi hizo zikaanzisha mafunzo mengine ya kijeshi. Aidha ni kwamba, wanachama wa kundi la Boko Haram wanajiunga na kundi hilo kutoka Nigeria, Niger, na Cameroon, huku kundi la ash-Shabab kwa upande wake likipata wanachama kutoka Somalia, Kenya, Ethiopia, Misri, Sudan na kadhalika. Mfumo huo ndio mfumo ule ule unaotumiwa na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh huko nchini Iraq na Syria. Kundi hilo nalo lilipata wanachama kutoka mataifa mbalimbali ya dunia na kuanzisha operesheni za pamoja zilizoambatana na utendaji jinai za kutisha dhidi ya binaadamu. Ni vyema ifahamike kwamba, katika ajenda za miaka 20 ya kundi la kigaidi la al-Qaidah, ilitangazwa kuwa, kati ya mwaka 2014 na 2016 kitakuwa kipindi cha kutangazwa dola la khilafa la makundi ya kigaidi. Kwa mujibu wa weledi wa mambo, ikiwa suala hilo litatimia, basi litapelekea kuibuka mlingano mpya wa kieneo na kusababisha mabadiliko ya makubwa katika eneo hili hasa kwa kuzingatia mahusiano yaliyopo baina ya makundi ya kigaidi kwenye kona mbalimbali za dunia.../mh