IQNA

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon

Nowruz ni fursa ya kipekee kwa watu kuungana na kuheshimiana

19:39 - March 20, 2015
Habari ID: 3015830
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amejiunga na taifa la Iran katika kuadhimisha siku kuu ya Nowruz ya kuwadia mwaka mpya wa Hijria Shamsia.

Katika ujumbe wake kwa mnasaba wa siku hii, Ban amesema kuadhimishwa Nowruz kila mwaka ni fursa ya kipekee kwa watu ili waweze kuungana, kuheshimiana  na kusherehekea kuwepo tamaduni anuwai.  Katika ujumbe wake kwa manasaba wa siku ya Nowruz, yaani Tarehe 1 Farvardin mwaka 1394 Hijria Shamsia inayosadifiana na 21 Machi 2015, Ban amesisitiza kuwa Nowruz ni wakati wa umoja na mshikamano wa kijamii. Ameongeza kuwa, Nowruz ya mwaka huu ina maana maalumu kwani Umoja wa Mataifa unajithidi kuhakikisha kunakuwepo na mustakabali endelevu kwa kuleta mlingano baina ya mazingira na watu wote sambamba na kueneza amani endelevu duniani. Wakati huo huo, jana Alkhamisi kulifanyika sherehe kubwa za siku kuu ya Nowruz katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York ambapo mabalozi na wawakilishi wa nchi mbali mbali duniani walishiriki. Mbali na Iran, Nowruz pia husherehekewa na watu wa mataifa mbali mbali hasa katika nchi za Jamhuri ya Azerbaijan, Kazakhstan, Kyrgyzstan, Tajikistan, Turkmenistan, Uzbekistan na pia sehemu za Uturuki, Iraq, Afghanistan, India na Pakistan. Halikadhalika katika baadhi ya maeneo ya pwani ya Afrika Mashariki hasa Zanzibar, Nowruz huadhimishwa japo kwa wakati tafauti na ule wa mwanzo wa machipuo hapa Iran. Siku hii kwa Waswahili ni maarufu kama Nairuzi au mwaka kogwa.../mh

3013789

 

captcha