Kwa mujibu wa Ali Zadmehr, mkuu wa mahusiano ya umma wa Filamu ya Muhammad Rasulullah SAW, filamu hiyo imeonyeshwa kwa wahakiki na wataalamu wanaoshiriki katika tamasha hilo la kimataifa. Filamu hiyo imeonyeshwa kwa mara ya kwanza kimataifa siku ya Alkhamisi katika ukumbi wa sinema wa Imperial na ilikuwa filamu ya kwanza kuonyeshwa katika tamasha hilo. Zadmehr ameongeza kuwa, Filamu ya Muhammad Rasulullah SAW imeonyeshwa pia Ijumaa katika ukumbi wa Odeon Canada. Filamu ya Muhammad Rasulullah SAW ndio filamu pekee iliyooneyshwa katika siku ya kwanza kati ya filamu zingine 47 zinazoonyeshwa katika tamasha hilo.
Filamu hiyo pia ilianza kuonyeshwa Alkhamisi hapa nchini Iran. Mtengeneza filamu ya Muhammad Rasulullah SAW anasema filamu hiyo inauonyesha Uislamu kama dini ya amani na urafiki.
Filamu ya Muhammad Rasulullah SAW imetengenezwa na mtengenza filamu mashuhuri wa Iran Majid Majidi na inasimulia kisa cha Mtume Mtukufu SAW na inaanzia kabla ya kuzaliwa mtukufu huyo. Filamu hiyo ya dakika 171 imetengenezwa kwa bajeti ya dola milioni 50 na imetajwa kuwa filamu iliyogharimu kiasi kikubwa zaidi cha fedha nchini Iran na kwamba ilichukua miaka mitano kuitengeneza.../mh