IQNA

Mtazamo

Kwa nini tuepuke kutamka au kuandika ‘Mtume wa Uislamu’

11:35 - May 26, 2023
Habari ID: 3477046
TEHRAN (IQNA) – Neno “mjumbe” (Rasul) maana yake ni mtu anayeleta ujumbe na kuukabidhi kwa wengine. Jambo la muhimu kuhusu mjumbe huyu ni nani aliyemtuma, sio alicholeta. Utakatifu wa Mtume Muhammad (SAW) ni kwa sababu alitumwa na Mwenyezi Mungu.

Muda mrefu uliopita, nilimtembelea mwalimu wangu ayeheshimika, Ayatullah Haj Seyyed Mohammad Ali Rouzati (1929-2012 Miladia), na aliniambia kuwa marehemu Amiri Firouzkouhi, maleng na mwanachuoni maarufu wa Iran, aliandika makala kuhusu kutokuwa sahihi kutamka au kuandika "Mtume wa Uislamu".

Mwanzoni, nilishangaa kusikia kwamba istilahi hii si sahihi, lakini baada ya kusoma makala hiyo, nilikubaliana na malenga huyo na mwalimu wangu niliyemheshimu. Alisema kwamba tusitumie istilahi hii isiyo sahihi popote pale, kwa sababu liliibuliwa na Wanazuoni wa Masomo  ya Mashariki maarufu kama Mustashrikin kwa Kiarabu au Orientalists kwa Kiingereza. Mustashrikin  aghalabu  huwa wazungu na si Waislamu lakini huwa wanajifunza kuhusu Uislamu na Waislamu kwa kina na wengi pia huwa wataalamu wa lugha ya Kiarabu.

Cha kusikitisha ni kwamba tumekuwa wazembe kiasi kwamba waandishi wetu wengi wametumia istilahi hii ya ‘Mtume wa Uislamu’  katika majina ya vitabu vyao. Pia, tumeona kwa miaka mingi kwamba istilahi hii isiyo  sahihi inatumika katika maandishi mengi kwenye vyombo vya habari au kuchapishwa kwenye vyombo vya habari. Istilahi hii isiyo sahuhi inatumika wakati ambao  istilahi sahihi  ni  "Mtume wa Mwenyezi Mungu"  au ‘Rasulullah’ ambayo imetumika katika Qur’ani Tukufu, Hadith, na vitabu vilivyoandikwa na wanazuoni maarufu Waislamu.

“Rasul al-Islam” au Mtume wa Uislamu ni istilahi  ambayo haina historia ya matumizi katika Uislamu. Hata leo, katika jamii  za Kiislamu na hasa miongoni mwa wanazuoni na mashekhe ni nadra kuona matumizi ya istilahi ya "Rasul al-Islam". Labda neno hili lisilo sahihi linatumiwa kwa makusudi na Waarabu Wamarxi au watu wasio na dini ambao wanapinga dini, na msomaji wa Kiarabu anaweza kusema iwapo mwandishi anatumia  "Rasul al-Islam" basi yamkini haamini kuwa Mtume Muhammad SAW ni Mtume wa Mwenyezi Mungi bali ni mtume wa Uislamu na kawaida wanaosema hivyo huwa hawaamini kuwa Uislamu ni dini ya Mwenyezi Mungu.

Tunachohitaji kukumbuka ni kwamba tunapotumia neno “Rasul”, tunamaanisha mjumbe na mwakilishi. Jambo la muhimu kuhusu mjumbe huyu ni nani aliyemtuma, sio alicholeta. Utakatifu wa Mtume ni kwa sababu alitumwa na Mwenyezi Mungu.  Katika Qur’ani Tukufu, Mwenyezi Mungu daima anasisitiza jambo hili, na ndiyo maana istilahi “Mtume wa Mwenyezi Mungu” au ‘Rasulullah’ hutumika katika aya za Qur’ani Tukufu

Kwa msingi huo katika Qur’ani Tukufu, tuna istilahi ya  "Mtume wa Mungu", lakini kwa bahati mbaya, katika baadhi ya maandishi ya Waislamu, tunaona kwamba istilahi hii Qur'ani imebadilishwa na maneno yasiyo sahihi kama vile ‘Mtume wa Uislamu’.

Ikiwa tutapuuza nukta kuwa Mtume Muhammad SAW ni Mtume wa Mwenyezu Mungu na badala yake kutumia istilahi hii ya  “Mtume wa Uislamu”, tunafanya kile ambacho Mustashrikin walitaka kwa kuibua istilahi hii isiyo sahih. Kwa dhati yao, Mustashrikin hawaamini kwamba Mtume Muhammad SAW ni Mtume wa Mwenyezi Mungu yaani Rasulullah na hivyo kutamka Rasulullah ni kinyume na imani zao zisizo za kidini au za kupinga dini.

Kwa hiyo waliibua istilahi ya “Mtume wa Uislamu”  ambayo kidhahiri inaonekana sahihi na yenye mvuto lakini katika maana yake halisi ni kutokuwa na imani ya Mwenyezi Mungu na  hivyo kwa mtazamo wao Uislamu pia si dini ya Mwenyezi Mungu.

Bila shaka, tunajua kwamba Waislamu wanaotumia neno “Mtume wa Uislamu”, hawapingi ukweli kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu bali aghalabu wanafanya hivyo kwa kutofahamu malengo ya Mustashrikin.

Nadhani uzembe huu ulianza wakati wa kufasiri  au kunukuu vitabu na makala za Mustashrikin bila ya kuzingatia na kujali na hivyo kueneza  malengo halisi ya maandishi, maneno, imani na mawazo yao.

 Makala hii iliandikwa kwa Kiajemi na Hujjatul Islam Rasul Jafarian na kuchapishwa kwenye tovuti ya  IQNA mnamo Mei 22, 2023.

3483679

captcha