IQNA

Mamilioni katika maombolezo ya Imam Hussein AS duniani

14:40 - October 25, 2015
Habari ID: 3393538
Mamilioni ya Waislamu katika nchi mbalimbali za dunia wameshiriki maombolezo ya Ashura kukumbuka tukio chungu la kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume mtukufu, Muhammad SAW, yaani Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib AS. Nchini Iran misafara na maandamano ya mamia ya maelfu ya watu inaendelea kushuhudiwa katika miji mbalimbali katika kukumbuka siku ya Ashura.

Hali kama hiyo pia inaonekana katika nchi za Lebanon, Bahrain, Kuwait na hata katika nchi zilizoko nje ya eneo la Mashariki ya Kati. Aidha katika nchi za Kiafrika kama vile Tanzania, Nigeria, Kenya, Misri, Senegal na Afrika Kusini kumefanyika hafla za maombolezo ya siku ya Ashura.
Hata hivyo, kitovu cha kumbukumbu ya Ashura ni katika ardhi takatifu ya Karbala ambapo mamilioni ya Waislamu wamekusanyika kumuomboleza mauaji ya mmoja wa mabwana wa mashahidi wa peponi. Maafisa wa Iraq wanasema kuwa wafanyaziara zaidi ya milioni sita walishiriki katika maombolezo ya Imam Hussein AS mjini Karbala.
Takribani miaka 1376 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, moja kati ya vita mashuhuri katika historia ya Kiislamu na ya mwanadamu, vilitokea baina ya majeshi ya haki na batili katika ardhi ya Karbala huko Iraq. Siku hii inajulikana kwa jina la Ashura. Katika siku hiyo mjukuu wa Mtume Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib AS, alisimama kishujaa na wafuasi wake waaminifu 72, kukabiliana na jeshi la batili ili kuilinda dini ya Allah. Hamasa ya Karbala ilikuwa dhihirisho la mambo mawili makuu. Kwanza ni ujasiri, ushujaa, moyo wa kujitolea, uaminifu pamoja na kuyapokea kwa moyo mkunjufu mauti ya kuuawa shahidi, sifa walizojipamba nazo wapiganaji wachache wa jeshi la haki wakiongozwa na Imam Hussein AS dhidi ya Yazid bin Muawiya. Pili ni upeo wa ukatili, udhalimu na unyama ulioonyeshwa na jeshi batili la Yazid bin Muawiya. Baada ya kupambana kishujaa, hatimaye mjukuu huyo wa Mtume Muhammad SAW aliuawa shahidi tarehe 10 Muharram ambayo hujulikana kama Ashura.

3393204

captcha