Msikiti huo unaojulikana kama Masjid al-Salaam ndio eneo pekee la ibada kwa Waislamu katika mji huo. Kamati ya msikiti huo imesema hujuma dhidi ya Masij al-Salaam ni dhihirisho la chuki kubwa dhidi ya Uislamu katika mji wa Peterborough. Meya wa mji huo mbali na kulaani kitendo hicho amesema tukio hilo linatia wasiwasi na linaonyesha ongezeko la watu wenye misimamo ya kufurutu ada miongoni mwa jamii ya Wakristo katika eneo hilo.
Huku hayo yakijiri, Waislamu nchini Ufaransa wameelezea wasiwasi wao kuhusu jinsi polisi wanavyoendesha uchunguzi kuhusiana na mashambulizi ya kigaidi ya Paris yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 130 siku tatu zilizopita. Waislamu katika mji mkuu wa Ufaransa wanasema wamekuwa wakipokea jumbe za kuwatishia maisha na licha ya kuripoti kwa polisi, hakuna hatua zozote zinazochukuliwa kuwalinda.