Mohammad Ali ametoa kauli hiyo kufuatia matamshi ya chuki dhidi ya Uislamu yaliyotolewa na Donald Trump anayewania kupata tiketi ya chama cha Republican kugombea kiti cha urais Marekani.
Katika taarifa, Mohammad Ali amesema: "Sisi kama Waislamu tunapaswa kusimama na kukabiliana na wale ambao wanatumia Uislamu kwa ajili ya ajenda binafsi. Hawa ni watu ambao wamepelekea wengi waache kujifunza Uislamu. Waislamu wa kweli wanafahamu kuwa hairuhusiwi kumlazimisha mtu awe Mwislamu."
Siku ya Jumatatu, Trump alisema 'Waislamu wanapaswa kuzuiwa kabisa kuingia Marekani." Alitoa matamshi hayo baada ya mauaji ya huko San Bernardino, California ambapo watu 14 walipoteza maisha. Watu wanaodaiwa kuwa na uhusiano na kundi la kigaidi la ISIS wanatuhumiwa kutekeleza hujuma hiyo ambayo imelaaniwa na Waislamu kote Marekani. Bingwa hiyo wa zamani wa masumbwi duniani alisashiria hujuma za kigaidi Paris Ufaransa na Marekani na kusema: "Mimi ni Mwislamu na hakuna mafundisho yoyote ya Uislamu yanayoruhusu kuuawa watu wasio na hatia Paris, San Bernardino au popote pale duniani. Waislamu wanafahamu kuwa ukatili wa wanojiita mujahidina ni kinyume kabisa cha misingi ya dini yetu."
Katika siku za hivi karibuni kumeshuhudiwa wimbi kubwa la chuki dhidi ya Uislamu huku Waislamu nchini humo na katika nchi zingine za Magharibi wakiingiwa na wasi wasi kuhusu usalama wao.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni uliofanywa Alhamisi na taasisi ya Gallup, asilimia 91 ya wapiga kura Marekani walisema wanamfahamu Trump lakini ni asilimia 32 tu walio na mtazamo mzuru kumhusu huku asilimia 59 wakimpinga.
Uchunguzi mwingine wa maoni uliofanya na Bloomberg Politics kupitia taasisi ya PulsePoll umebaini kuwa asilimia 65 ya Warepublican wanamuunga kono Trump katika matamshi yake dhidi ya Waislamu.