
Katika mkutano huo, Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei aligusia umuhimu
wa suala la sanaa na kuelezea kufurahishwa kwake na kuona kuwa chuo
kikuu cha kidini kimeingia katika uga wa fikihi ya sanaa na kuongeza
kuwa, sanaa, ni kitu kilichobarikiwa cha kibinadamu na ni matunda ya
kuwa na tafakuri pana, hisia na dhuku kali na ni sehemu ya maisha ya
mwandamu. Amesema, kati ya wanavyuoni na mafakihi wa hawza (vyuo vikuu
vya kidini) kumejaa watu waliobobea katika sanaa na ambao ni majimbi
katika bahari za tungo na fasihi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya
Kiislamu aidha amesema ni jambo la dharura na lenye baraka nyingi la
kufanya uhakiki, kupiga mbizi na kubainisha vizuri fikihi ya sanaa
katika jamii. Ameongeza kuwa, fikihi ndiyo inayosimamia mambo yote
katika maisha ya mwandamu na sanaa ni moja na mambo hayo ambayo fikihi
inapaswa kuyashughulikia.
Amesema, kazi ya kuchunguza, kuhakiki,
kufanya utafiti na hatimaye kutoa hukumu na nadharia za kifikihi
kuhusiana na sanaa ni kazi ambayo inahitajia kuwa na utambuzi wa kina
kuhusiana na sanaa, mipaka na hududi zake.
Amesema, Uislamu si tu
kwamba unakubaliana na sanaa, bali hata unashajiisha kufanya kazi za
sanaa, na mifano mingi ya sanaa katika historia ya Uislamu ni
uthibitisho wa namna dini hiyo ya Mwenyezi Mungu inavyolipa umuhimu
suala la sanaa na kuhamasisha kufanyiwa kazi.
Ayatullah Udhma
Khamenei ameashiria namna sanaa ilivyojikita vilivyo katika jamii za
mwanadamu leo hii na athari zake za moja kwa moja katika fikra, roho na
mtindo wa maisha ya watu na kuongeza kwa kusema: Amma kuhusiana na
baadhi ya fatwa maarufu kuhusu masuala ya sanaa ni kwamba inawezekana
kuja na fatwa mpya kwa kupiga mbizi na kuzama zaidi katika fikihi.
Kiongozi
Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuhusu mambo ya lazima ya
kuja na vitu vipya katika fikihi ya sanaa kwamba: Inabidi usuli na
misingi ya fikihi ichungwe kikamilifu katika suala hilo na inabidi
hukumu na fatwa zitolewe kwa kutumia usuli na msingi wa kutoa fatwa wa
wanavyuoni wa Kishia na kwa kutegemea Qur'ani na Sunna, bila ya
kuathiriwa na wimbi na anga inayotawala katika jamii.
Aidha amesifu
hatua ya kuanzisha sunna nzuri ya kuiingiza fikihi katika sanaa na
kuitisha kongamano la fikihi ya sanaa na amewasisitizia waendeshaji na
wasimamiaji wa kongamano hilo kwa kuwaambia: Kazi hii ilipaswa ianze
zamani sana na kwa vile hivi sasa imeshaanza, inabidi iendelee bila ya
kusita.
3467109