IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Marekani inatoa misaada kwa magaidi

22:33 - April 12, 2016
Habari ID: 3470244
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema misaada ya silaha na kifedha inayotoa Marekani kwa makundi ya kigidi ni moja ya vizuizi katika utatuzi wa tatizo la ugaidi.

Ayatullahil Udhma Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo leo Jumanne mjini Tehran katika mkutano wake na Matteo Renzi Waziri Mkuu wa Italia. Kiongozi Muadhamu ameongeza kuwa, kuna habari zenye ushahidi wa kutosha kuwa Marekani inatoa msaada kwa magaidi wa ISIS au Daesh na makundi mengine ya kigaidi. Ameongeza kuwa hata hivi sasa wakati kumeundwa muungano wa kupamabana na ISIS baadhi ya taasisi za Kimarekani zinatoa msaada kwa magaidi wa ISIS.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, vyombo vikubwa vya habari duniani, ambavyo vinadhibitiwa na watawala wa nchi za Magharibi, vinatumia kisingizio cha vitendo vya wahalifu wachache na magaidi ili kueneza chuki dhidi ya Uislamu.

Kwingineko katika matamshi yake, Ayatullah Khamenei amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inakaribisha kuimarisha uhusiano na Italia katika nyanja mbali mbali hasa za ushirikiano wa kiuchumi. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria uhusiano mzuri wa Iran na Italia na kusema, mtazamo wa Iran kuhusu ushirikiano na Italia na serikali ya nchi hiyo ni mtazamo tafauti na chanya.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema muamala wa Italia katika zama za vikwazo vya kulazimishwa dhidi ya Iran ulikuwa muamala wa kimantiki zaidi ya nchi zingine za Magharibi. Amesema baadhi ya serikali na mashirika ya Ulaya yanakuja Iran na kufanya mazungumzo lakini hadi sasa matokeo ya mazungumzo hayo hayajabainika.

Kiongozi Muadhamu amesema kupambana na ugaidi ni kati ya sekta nyingine ya ushirikiano wa Iran na Italia. Ameongeza kuwa, nchi kadhaa za Ulaya zimekuwa zikiunga mkono makundi hatari ya kigaidi na leo wimbi hatari na pana la ugaidi limefika Ulaya.

Kwa upande wake, Matteo Renzi Waziri Mkuu wa Italia ameashiria irada ya nchi yake ya kuimarisha uhusiano na Iran na kusema, 'mapatano ya nyuklia yanapaswa kupelekea Iran kuondolewa vikwazo.'

Aidha amebainisha masikitiko yake kuhusu kuenea ugaidi Ulaya. Kuhusu kuuharibia jina Uislamu kwa kisingizio cha ugaidi, amesema ifahamike kuwa dini zinataka amani , mazungumzo na watu kuishi pamoja. Aidha amepongeza nafasi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika kueneza mtazamo huo na kuitaja nukta hiyo kuwa muhimu sana.

3488133

captcha