IQNA

Mtaalamu wa Qur'ani kutoka Algeria

Mashindano ya Qur'ani ya Iran ni ya kipekee

18:13 - April 24, 2017
Habari ID: 3470949
TEHRAN (IQNA)-Mtaalamu wa masuala ya Qur'ani kutoka Algeria amesema mashindano ya kimataifa ya Qur'ani ya Iran mwaka huu ni ya kipekee na ya aina yake duniani.

Katika mahojiano maalumu na IQNA, Sheikh Omar bin Ahmed Busaada ambaye yuko katika jopo la majaji katika Mashindano ya 34 ya Kimataifa ya Qur'ani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuandaa mashindano matano kwa wakati moja ni jambo linalohitaji jitihada na usimamizi bora.

Katika mashindano ya kimataifa ya Qur'ani yaliyofunguliwa rasmi Jumatano iliyopita na kuanza Alhamisi mjini Tehran, mbali na yale ya kila mwaka ya wanaume ya kuhifadhi na kusoma Qur'ani, mwaka huu pia kuna mashindano maalumu ya kimataifa ya Qur'ani ya wanawake, watu wenye ulemavu wa macho, wanacuo wa vyuo vikuu vya kidini na yale ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari. Halikadhalika mbali na mashindano hayo kuna kongamano la kimataifa kuhusu masomo ya Qur'ani na pia maonyesho ya bidhaa zinazohusiana na Qur'ani Tukufu.

Sheikh Busaada amesema katika baadhi ya nchi kunafanyika mashindano kadhaa ya kitaifa lakini hii ni mara ya kwanza kushuhudiwa mashindano ya kimataifa ya vitengo mbali mbali.

Mwanazuoni huyo wa Algeria amepongeza hatua ya Iran kuwaleta pamoja wasomaji na wenye kuhifadhi Qur'ani kutoka nchi mbali mbali za Kiislamu na hata zisizo za Kiislamu na kuongeza kuwa ni jambo lenye faida kubwa kwa Waislamu wa mataifa mbali mbali kukutana kwa ajili ya Qur'ani Tukufu.Mashindano ya Qur'ani ya Iran ni ya kipekee

Mtaalamu huyo wa Qur'ani kutoka Algeria katika tathmini yake kuhusu uwezo wa washiriki wa kitengo cha Tajwidi amesema wengi wana kiwango cha wastani kwa mtazamo wa Waqf na Ibtida na hivyo ametoa wito kwa quraa na wasomi wa Qur'ani kujitahidi katika mawili hayo sambamba na kuzingatia kanuni zinginezo za Tajwidi.

Sheikh Busaada amewahi kuwa jaji katika mashindano ya Qur'ani katika nchi yake Algeria na pia Morocco, Tunisia na Ufaransa. Amesema mwaka huu yeye ni jaji katika mashindano ya Qur'ani nchini Iran lakini aliwahi kuja Iran kama mwakilishi wa Algeria katika mashindano ya kimataifa ya Qur'ani.

3592659
captcha