Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, ameyasema hayo asubuhi ya leo mjini Tehran alipokutana
na walimu, maqarii na mahufadhi wa Qur'ani Tukufu walioshiriki
katika Mashindano ya 34 ya Kimataifa ya Qur'ani nchini hapa kutoka nchi
83 za dunia. Amesema kuwa utambulisho wa Kiislamu unazuia uingiliaji na
ubeberu wa maadui na kuongeza kuwa, mafundisho ya Qur'ani, ni muokozi na
mjengaji wa maisha ya uwezo imara na ya izza kwa umma wa Kiislamu na ni
lazima mafundisho hayo yawekwe wazi na kuenezwa katika jamii ya
Kiislamu. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, amesema kuwa, kinachoutanza hii leo umma wa Kiislamu ni "ubeberu wa kiutamaduni, kiuchumi na kisiasa wa Magharibi" na akafafanua kwamba, leo hii nchi nyingi za Kiislamu hazina "Utambulisho wa Kiislamu", na maadui wanaweza kuingilia utamaduni, imani, uchumi, siasa na mahusiano yao ya kijamii na kuchochea vita na chuki baina ya Waislamu.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema kuwa, kujiweka mbali na Qur'ani kunatoa mwanya kwa maadui wa kupandikiza mbegu za utovu wa imani na utegemezi; na akabainisha kwamba hali ziliyonayo leo serikali za nchi za Kiislamu mkabala na Marekani, Uzayuni na waporaji, inatokana na serikali hizo kujiweka mbali na Qur'an kwani ikiwa tutajikurubisha na kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu na utambulisho wa Kiislamu, matatizo yote haya yataondoka.
Kadhalika Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, juhudi za kuieneza na kuifahamu Qur'an, ni moja ya mema makubwa kabisa ambapo sambamba na kusisitiza juu ya udharura wa kuendelezwa harakati za masuala ya Qura'ni nchini Iran amesema kuwa, ni jambo la kusikitisha kuwa mataifa ya Waislamu na nchi za Kiislamu zimejiweka mbali na kitabu hicho cha mbinguni na hazina uelewa wa mafundisho yake halisi. Amesema kuwa, "Kumpinga Taghuti na Kumwamini Mwenyezi Mungu" ni moja ya maana muhimu na yenye kujenga utambulisho ya Qur'an na kwamba, kutiliwa mkazo "Utambulisho wa Kiimani" kuna maana ya kuwekwa mpaka na kujitegemea ili utambulisho huo uweze kujilinda katika kukabiliana na "Utambulisho wa Taghuti na Ukafiri" na kuendelea kupiga hatua zake za maendeleo.


