IQNA

Wakimbizi Milioni moja Waislamu Warohingya wapata hifadhi Bangladesh

11:41 - October 29, 2017
Habari ID: 3471237
TEHRAN (IQNA)-Afisa wa Hilali Nyekundu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (ICRS) amesema kuna takribani wakimbizi zaidi ya milioni moja Waislamu wa jamii ya Rohingya waliokimbia mauaji ya kimbari Myanmar na kuingia nchini Bangladesh.
Wakimbizi Milioni moja Waislamu Warohingya wapata hifadhi BangladeshAhmad Soltani, Mkuu wa Mipango na Elimu Maalumu katika ICRS amesema hakuna idadi rasmi iliyotangazwa lakini kwa makadirio yake, Waislamu Warohingya waliovuka mpaka kutoka Myanmar na kuingia Bangladesh ni takribani milioni 1.2.

Soltani ameyasema hayo katika warsha ya 'Athari Mbaya za Mauaji ya Kimbari Myanmar' ambalo lililofanyika Jumamosi katika Maonyesho ya 23 ya Vyombo vya Habari ya Tehran. Kibanda cha IQNA katika maonyesho hayo kilikuwa mwenyeji wa warshi hiyo.

Halikadhalika Soltani amesema kuwepo idadi kubwa ya wakimbizi Warohingya nchini Bangladesh kunamaanisha kuwa aghalabu ya Waislamu Warohingya tayari wameshaondoka Myanmar kufuatia mauaji ya kimbari nchini humo.

Afisa huyo wa Hilali Nyekundu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Waislamu Warohingya wamekuwa wakikandamizwa kwa muda mrefu nchini Myanmar na haipaswi kunyamazia kimya jinai hiyo.

Aidha amesema jamii ya kimataifa inapaswa kuishinikiza Myanmar ili wakimbizi Warohingya warejee katika makao yao ya jadi katika jimbo la Rakhine.

Soltani amesema Hilali Nyekundu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inashirikiana na mashirika mengine ya kimataifa katika kutoa misaada kwa Waislamu Warohingya ambao wanahitaji makazi, maji safi, chakula, nguo na huduma za afya. Aidha amesema Irna tayari imeshatuma shehena tatu za misaada kuwasaidia Waislamu Warohingya nchini Bangladesh. Soltani ameongeza kuwa ICRS inashirikiana na Wizara ya Afya ya Iran kujenga hospitali ya muda na kliniki tano kuwasaidai Warohingya katika kambi za wakimbizi nchini Bangladesh.

Taarifa zinasema tokea Agosti 25 wakati Jeshi la Myanmar lilipoanzisha hujuma dhidi ya Waislamu katika jimbo la Rakhine, Waislamu zaidi ya elfu sita wameuawa kwa umati na wengine elfu nane wamejeruhiwa.

Katika miaka ya karibuni, Waislamu wengi wa kabila la Rohingya nchini Myamnar wameuawa au kulazimika kuhama makazi yao na kuwa wakimbizi katika nchi za jirani kutokana na mashambulio ya Mabuddha wenye misimamo ya kufurutu mpaka wanaoungwa mkono na serikali ya nchi hiyo.

3464279


captcha