IQNA

11:37 - August 27, 2019
News ID: 3472102
TEHRAN (IQNA) - Wakimbizi wapatao laki mbili Waislamu wa jamii ya Rohingya wa nchini Myanmar Jumapili walishiriki kwenye kumbukumbu ya mwaka wa pili tangu jeshi la Myanmar lilipowakandamiza na kuwalazimisha kuyahama makazi yao kwa umati na kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh ili kunusuru maisha yao.

Waislamu hao wameadhimisha kumbukumbu hiyo kwa maandamano ya amani na dua zilizofanyka kwenye kambi ya Kutupalong iliyoko kwenye eneo la Bazar ya Cox nchini Bangladesh.

Umati mkubwa wa Waislamu hao ulijumuisha watoto wadogo, wanawake waliovalia vazi la staha la Kiislamu la Hijabu pamoja na wanaume, ambao kwa pamoja walipaza sauti zao kutoa nara za: "Allah ndiye mkubwa kabisa, Rohingya waishi umri mrefu", katika maandamano hayo yaliyofanyika kwenye kambi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani, kuadhimisha ile waliyoielezea kama "Siku ya Mauaji ya Kimbari". Halikadhalika Waislamu hao waliwaombea dua wenzao waliouawa katika ukandamizaji wa kinyama uliofanywa na jeshi la Myanmar miaka miwili iliyopita.

Umoja wa Mataifa uliitaja hujuma hiyo iliyojumuisha ubakaji, mauaji, na uchomaji moto kikamilifu wa vijiji uliofanywa na askari ya Myanmar kuwa ni "kitabu cha kiada cha mfano wa uangamizaji wa kizazi."

Baadhi ya Waislamu hao Warohingya walibeba mabango na maberamu yenye maandishi yanayotoa wito kwa serikali ya Myamnar kuwapatia uraia wao na haki zao zingine kabla ya kukubali kurudi nchini kwao.

Agosti 25 mwaka 2017 Waislamu wapatao 740,000 wa jamii ya Rohingya walilazimika kuyahama makazi yao kwa umati katika jimbo lao la Rakhine na kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh walikojiunga na wenzao wengine laki mbili waliokuweko nchini humo, baada ya vikosi vya jeshi la Myanmar kuanzisha wimbi kubwa la hujuma na ukandamizaji dhidi ya Waislamu hao.

Maandamano ya Jumapili yalifanyika siku kadhaa baada ya jaribio la pili lililofeli la kuwarejesha wakimbizi hao, ambalo halikushuhudia hata Mrohingya mmoja aliyevuka mpaka kwa hiari na kurejea Myanmar.

Aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad Al Hussein amesema kuwa uhalifu unaofanywa na Mabudha kwa himaya ya serikali nchini Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya ni mauaji ya kimbari.

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, imesema inatafakari kuhusu kuanzisha uchunguzi kuhusu ukatili wanaotendewa Waislamu wa jamii ya Rohingya.

3469259

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: