IQNA

20:20 - December 05, 2019
News ID: 3472258
TEHRAN (IQNA- Imam Hasan al Askari AS ni Imam wa 11 wa Waislamu wa Madhehebu ya Shia na alizaliwa mwaka 232 Hijria mwezi 8 Mfunguo Saba Rabiuth Thani katika mji mtakatifu wa Madina.

Imam huyo alipata umaarufu wa kuitwa al Askari kutokana na kwamba aliishi na baba yake Imam Hadi AS katika eneo la Askar huko Samarra, Iraq, kwa amri ya makhalifa wa Bani Abbas. Kun’ya yaani jina lake la ubaba ni Abu Muhammad, na lakabu zake maarufu ni an Naqi na az Zaki. Mtukufu huyo alichukua Uimamu wa kuongoza umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake Imam Hadi AS. Na kwa vile hivi sasa tumo katika maadhimisho ya siku ya kuzaliwa mtukufu huyo, tunaitumia fursa hii kutoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba huo tukitaraji mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi.

Malengo ya Mitume na Manabii

Moja ya malengo makuu ya kutumwa Mitume na Manabii kwa mujibu wa aya za Qur’ani Tukufu ni kusimamisha usawa na uadilifu. Jambo hilo linalifanya suala la kuwepo viongozi na Maimamu waadilifu katika jamii wakati wote, kuwa jambo la dharura. Kwa mujibu wa aya ya 25 ya Suratul Hadid, inabidi aweko Kiongozi na Imam katika jamii wa kuwaongoza watu kwa mujibu wa sheria na kanuni za Mwenyezi Mungu na za Kiislamu kama njia ya kuweza kusimamishwa usawa na uadilifu duniani. Aidha imepokewa hadithi kutoka kwa Imam Ridha AS akisema: Moja ya dalili na sababu za udharura wa kuweko Imam na Kiongozi ni kwamba jamii inahitajia kuwa na sheria, na watu katika jamii wana jukumu na ulazima wa kuheshimu sheria, kwani kuvunja mipaka hiyo hupelekea kufisidika jamii na pia kunahitajika mlinzi mwaminifu wa kuweza kulinda sheria, vinginevyo hakuna mtu ambaye yuko tayari kuachana na starehe na manufaa yake binafsi hata kama yatapelekea kufisidika jamii. Hivyo Mwenyezi Mungu anamteua mja Wake mmoja na kumkabidhi jukumu la kusimamia mambo ya watu ili azuie ufisadi na uharibifu wa mafisadi na waharibifu katika ardhi, na vile vile kuhakikisha mfumo wa sheria una nguvu na unasimamia nukta zote za maisha ya jamii. Dalili nyingine ya udharura wa kuweko Mitume na Maimamu katika jamii ni kwamba hakuna kundi wala taifa lolote linaloweza kuishi bila ya kuwa na msimamizi na kiongozi wa kusimamia masuala ya kidini na kidunia ya jamii hiyo, masuala ambayo jamii yoyote ile haiwezi kukwepa kuyatekeleza. Hivyo hekima ya Mwenyezi Mungu Mwingi wa busara hairuhusu awaache viumbe Wake vivi hivi bila ya kuwawekea kiongozi ambaye ataweza kusimamia masuala ya dharura kama hayo.

Udharura wa kuweko Imam katika jamii

Naye Imam Sadiq AS amesema kuhusu udharura wa kuweko Imam katika jamii kwamba: Ardhi kamwe haiwezi kubakia tupu bila ya Imam. Imam inabidi awepo wakati wote ili pale watu walioamini wanapoongeza kitu katika dini aweze kuwarejesha kwenye uhalisia wa dini na kama watapunguza kitu katika dini aweze kuwakumbusha na kukirejesha.

Mifano ya uhakika huo wa kimantiki imeonekana sana katika historia ya mwanadamu. Viongozi na Maimamu katika jamii wapo kwa ajili ya kuleta nidhamu kwenye maisha ya mwanadamu na kumuongoza katika njia ya mafanikio na ufanisi na kusimamia masuala ya mtu mmoja mmoja na ya jamii nzima kiujumla na kuwa mithili ya taa inayong’ara ya kuwaongoza watu katika uongofu. Viongozi hao sambamba na kuwafundisha watu mafundisho asili ya Uislamu wana jukumu pia la kuwaonyesha watu njia sahihi ya kifikra na kumwokoa mwanadamu kutokana na upotofu wa kifikra, mazingira anayoishi, taasubu, kufuata mambo kibubusa na kutekwa na matamanio ya kinafsi. Ukweli wa mambo ni kuwa kuwepo Imam katika jamii ndilo sharti la kuweza kupatikana ufanisi na ubora katika maisha ya watu. Mtu ambaye anao uwezo wa kumzuia dhalimu kufanya dhulma yake na mtu ambaye anao uwezo wa kuwaongoza kikwelikweli watu katika ibada ya Mungu Mmoja, kuwa na imani thabiti na kupambana na ufisadi katika jamii, ni Imam maasumu.

Imam Sadiq AS amesema: Imam kwa watu ni shahidi na ni mlango wa Mwenyezi Mungu na ni njia ya kuelekea kwa Allah na ni mfasiri wa wahyi. Imam ana nguvu za muujiza na dalili madhubuti na ni mithili ya nyota kwa wakazi wa mbinguni na wameteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa Maimamu kwa ajili ya kuwalinda na kuwaongoza watu hapa ardhini. Maimamu ni mfano wa merikebu ya Nuh, yeyote anayepanda merikebu hiyo huokoka na kufika salama ufukweni.

Imam Hasan al Askari AS, Nuru iliyochomoza

Imam Hasan al Askari ni miongoni mwa Maimamu hao wateule wa Mwenyezi Mungu ambaye kuzaliwa kwake kulikuwa ni sawa na kuchomoza nuru katika maisha ya wanadamu waliochoshwa na dhulma na ukandamizaji. Imam Askari AS ni kutoka kizazi kitoharifu cha Bwana Mtume Muhammad SAW ambacho Bwana Mtume amesema kwenye hadithi yake maarufu kwamba Ahlul Bayt wake hawatotengana na Qur’ani Tukufu hadi siku ya kiyama. Akielezea nafasi ya Maimamu na Ahlul Bayt wa Bwana Mtume Muhammad SAW, Imam Askari AS amenukuliwa akisema: Sisi tumeweza kufikia vilele vya juu kabisa vya uhakika kutokana na kuweko kwetu Unabii na Wilaya…

Imam Hasan al Askari AS ni muendelezo wa uogozi wa waja wema kwa ajili ya kuleta nidhamu katika umma wa Kiislamu na kuzifanya amri za Mwenyezi Mungu zitekelezwe kivitendo. Alichukua Uimamu akiwa na umri wa miaka 22 kwa ajili ya kuwaongoza watu kuelekea kwenye uongofu na kutii amri za Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Katika kipindi cha miaka 28 ya maisha yake yaliyojaa baraka, Imam Askari AS aliwarithisha wanadamu mambo mengi ya thamani. Tangu akiwa mdogo, alilazimika kuhama Madina akiwa na baba yake Imam Hadi AS na kupitisha sehemu kubwa ya umri wake chini ya udhibiti wa maafisa wa utawala wa Bani Abbas kwenye mji wa Samarra, (Iraq ya leo) katika eneo la kijeshi. Hata hivyo, kubaidishwa mtukufu huyo hakukumzuia kuwa na mawasiliano ya karibu na watu na kupata wafuasi wengi waaminifu. Hapa pana kisa kifupi kilichohadithiwa na mmoja wa wafuasi maarufu wa Imam Hasan al Askari AS.

Ukarimu

Abu Hashim Jaafari anasimulia kwamba: Siku moja nilibanwa na ukata na umaskini na nikataka kuomba dinari kadhaa kutoka kwa Imam Hasan Askari AS. Nilimwendea mtukufu huyo lakini nikashindwa kusema lolote kwa kuona soni, na baadaye nikarejea nyumbani. Hata hivyo Imam alielewa matatizo yangu. Muda mfupi baadaye mjumbe wa Imam Askari alibisha hodi na kunipa dinari mia moja kutoka kwa mtukufu huyo pamoja na ujumbe uliokuwa na maandishi yafuatayo: Uwapo na haja usiwe na haya na woga wa kusema. Omba unachotaka, utapewa."

Amma kuhusiana na umuhimu wa kutambua haki za ndugu katika dini na kuwa mpole mbele yao, Imam Askari amenukuliwa akisema: "Mtu anayetambua zaidi haki za ndugu zake hufanya juhudi kubwa zaidi za kutekeleza haki hizo na kuwa na nafasi ya juu kwa Mwenyezi Mungu. Mtu mpole kwa ndugu zake duniani atakuwa pamoja na siddiqin kwa Mola Mlezi.

Kutosalimu amri mbele ya madhalimu

Amma moja ya sifa makhsusi za maisha ya Imam Hasan al Askari AS ni kutosalimu amri mbele ya madhalimu na madikteita na kusimama kwake imara katika njia ya haki. Mbali na jukumu lake kubwa la kuwaongoza watu katika kipindi cha Uimamu wake, Imam alikuwa na jukumu jingine ambalo ni kutayarisha Umma kwa ajili ya kipindi cha ghaiba ya Imam Mahdi AS. Kwani Imam wa Zama na Mwokozi Aliyeahidiwa wa walimwengu ni mwana wa Imam Hasan al Askari na alianza kipindi cha ghaiba ndogo baada tu ya kumalizika kipindi cha uongozi wa baba yake. Katika kipindi hicho kilichojaa ukandamizaji, maisha ya mwana huyo wa Imam Askari yalitishiwa na watawala madhalimu wa Bani Abbas. Hata hivyo Imam Mahdi AS alisalimika na njama za watawala hao kwa rehema zake Mola Muweza na tadibiri ya Imam Hasan al Askari AS.

Tukiendelea na kutupia jicho miongozo yake mitukufu, Imam Hasan al Askari alikuwa analihesabu suala la kuzidisha welewa na muono wa mbali wa watu kuwa ni jambo muhimu mno. Katika moja ya hadithi zake amenukuliwa akisema: Ibada si kufunga saumu sana na wala kusali sana tu, bali ibada ya kweli ni kuzidisha kumkubuka Allah (kwa dhati na kwa wakati wote).

Vile vile amesema katika hadithi nyingine kwamba: Sura ya wema ni ujamali wa dhahiri na akili na tafakuri ya wema ni ujamali wa batini.

Kumtambua Allah kwa ikhlasi

Imam Askari AS alikuwa akilihesabu sharti la kufanikiwa katika migogoro na changamoto zinazojitokeza mara kwa mara na kuweza kuzidhibiti vilivyo changamoto hizo, ni kumtambua Allah, kuwa na ikhlasi katika matendo na kujiweka mbali na tashiwishi za upotofu. Siku zote alikuwa akiwahimiza wafuasi wake wawe makini muda wote katika fikra na matendo yao, na mara zote wajiepushe na matendo yote yasiyo sahihi.

Kutokana na kuwa kwake Imam maasumu, Imam Hasan al Askari AS kamwe hakuwahi kufanya jambo kwa matamanio ya nafsi, bali matendo yake yote yalizingatia misingi na usuli maalumu zilizotokana na mafundisho ya Qur’ani Tukufu. Ni kwa sababu hiyo ndio maana fikra, maneno na matendo ya mtukufu huyo yakawa ni kigezo bora cha kufuatwa katika maisha yote ya wanadamu na katika sehemu yoyote ile na kwenye zama zote ziwazo. Alikuwa akihimiza mno suala la ucha Mungu na kujipamba kwa sifa bora.

Tunatoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kuzaliwa Imam Hasan al Askari AS.

/3861810/

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: