Katika kikao na balozi mpya wa Uswidi (Sweden) nchini Misri, Sheikh al-Tayeb alisema kuwa matendo ya kukufuru Qur’ani Tukufu, ambayo yameshuhudiwa nchini Uswidi na baadhi ya mataifa mengine katika miaka ya karibuni, yameumiza hisia za Waislamu wapatao bilioni mbili duniani, ikizingatiwa utukufu wa Qur’ani kwa Umma wa Kiislamu.
Alisisitiza haja ya kuchukua hatua madhubuti ili kuzuia kurudiwa kwa matendo kama hayo, ambayo hayawezi kuhalalishwa kwa kisingizio cha “uhuru wa kujieleza."
Sheikh al-Tayeb alieleza kuwa hakuna uhuru wa kutoa matusi dhidi ya maeneo matakatifu ya dini. Akiwa amejaa huzuni, alihoji uhusiano kati ya uhuru wa kujieleza na matusi dhidi ya dini na vitabu vitakatifu, akisema kuwa kuendelea kwa matendo hayo kunatishia maadili ya kibinadamu na kuchochea chuki katika jamii.
Imamu Mkuu wa Al-Azhar alisisitiza kuwa serikali zinapaswa kuzuia ukiukaji huo na kutunga sheria kali za kuzuia, kwani ni jukumu kubwa linalopaswa kutekelezwa kwa dhati.
Kwa upande wake, balozi mpya wa Uswidi mjini Cairo, Dag Bolin Dunfleet, alisifu juhudi za Sheikh wa Al-Azhar katika kuendeleza maadili ya uvumilivu na kuishi kwa amani, na kusema kuwa watu wa Uswidi wanaheshimu dini zote na wanapinga vikali vitendo vyovyote vya chuki dhidi ya Uislamu.
Balozi huyo pia alieleza kuwa Waislamu wanawakilisha takriban asilimia 10 ya idadi ya watu wa Uswidi na ni sehemu muhimu ya jamii ya Uswidi. Alionyesha matumaini kuwa matukio kama hayo hayatarudiwa tena siku za usoni.
4310564