IQNA

21:46 - April 20, 2021
News ID: 3473833
TEHRAN (IQNA)- Nara ya Siku ya Kimataifa ya Quds mwaka hii itakuwa ni “Tunakaribia Quds Zaidi ya Wakato Wowote Mwingine”.

Hayo yametangazwa na Hujjatul Islam wal Muslimin Mohammad Hassan Akhtari, mwenyekiti wa Kamati ya Kuunga Mkono Mapinduzi ya Kiislamu ya Watu wa Palestina.

Akizungumza na waandishi habari mjini Tehran, amesema maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds ambayo yamekuwa yakifanyika kila mwaka katika zaidi ya nchi 100 duniani yamepelekea kadhia ya Palestina kuwa kadhia muhimu zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu hivi leo.

Ameongeza kuwa, mwaka huu, kutokana na janga la COVID-19, hakutakuwa na maandamano au mijumuiko ya aina yoyote.

Hujjatul Islam wal Muslimin Mohammad Hassan Akhtari amesema mwaka huu harakati za kutetea ukombozi wa Palestina na kulaani utawala wa Kizayuni wa Israel unaokalia ardhi za Palestina zitafanyika katika mitandao ya kijamii na intaneti.

Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu hayati Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu) ndiye aliyeipa siku hiyo ya Ijumaa ya mwisho ya mwezi Ramadhani jina la Siku ya Kimataifa ya Quds kwa shabaha ya kuakisi dhulma ya kihistoria inayofanywa na madola ya Magharibi yanayodai kutetea haki za binadamu, dhidi ya watu wanaoendelewa kudhulumiwa na kukandamizwa wa Palestina na ardhi yao takatifu. Tokea ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran mwaka 1979, Siku ya Kimataifa ya Quds imekuwa ikiadhimishwa kupitia maandamano na makongamano  kote duniani.

3965946

Name:
Email:
* Comment:
* captcha: