IQNA

Shakhsia katika Qur'ani /20

Watoto wa Nabii Yakub (AS)

20:57 - December 12, 2022
Habari ID: 3476237
TEHRAN (IQNA) – Baada ya Nabii Yakub, Amani ya Mwenyezi Mungu Iwe Juu Yake,- AS- kujulikana kama Isra’il, familia yake na watoto wake waliitwa Bani Isra’il (wana wa Isra’il). Watoto na vizazi vyake wengi waliishi Misri na Palestina.

Baada ya kuhimizwa na  baba yake, Yakub (AS) alioa wasichana wawili kutoka Mesopotamia ambao walikuwa wameokoka gharika iliyowakumba watu wa Nabii Nuh. Uliya na Raheel yalikuwa ni majina ya wake zake. Katika masimulizi ya kihistoria, Bilha na Zulfa wametajwa kama wake zake wengine wawili. Yakub (AS) alikuwa na watoto 12 ambao miongoni mwao ni Yusufu pekee (AS) alikua Nabii.

Watoto wa Yakub (AS) wote walikuwa hodari, washupavu na wazuri, huku Yusufu (AS) akiwa ni mzuri zaidi miongoni mwao. Yakub alimpenda zaidi kuliko watoto wake wengine. Ndiyo maana Yusuf alionewa wivu na kaka zake tangu utotoni.

Ndugu za Yusudf walimtupa ndani ya kisima na kumwambia baba yao kwamba mbwa-mwitu amemla. Lakini Yusufu aliokolewa na kufika Misri na hatimaye akatawala nchi hiyo kwa muda fulani.

Kulingana na vyanzo vya Kiislamu, mwana wa kwanza wa Yakub aliitwa Sham’un. Alikuwa mtu mwenye hekima na aliwaongoza ndugu zake wengine. Baadhi ya wafasiri wa Qur'ani Tukufu wanasema Sham’un alipinga wazo la ndugu wengine kumuua Yusuf na akapendekeza atupwe kisimani.

Katika baadhi ya simulizi za kihistoria ingawa Reuben au Roubin ametajwa kuwa mwana mkubwa wa Yakub. Alikufa akiwa na umri wa miaka 135 na akazikwa huko Palestina.

Lawi alikuwa mtoto wa tatu wa Yakub. Anachukuliwa kuwa babu wa Omran na babu mkubwa wa Musa (AS). Alienda Misri pamoja na baba yake na kukaa huko hadi akafa akiwa na umri wa miaka 137.

Yehuda (Yuda) alikuwa mwana wa nne wa Yakub. Anachukuliwa kuwa babu mkubwa wa Daudi (AS) na Issa au Yesu (AS). Wengine wanaamini kwamba neno Myahudi linatokana na jina lake.

Dani na Naftali walikuwa wana wa tano na wa sita. Vizazi vyao viliishi kaskazini mwa Palestina. Gad alikuwa mwana wa saba na alikuwa na wana saba, ambao kila mmoja aliongoza kabila moja. Waliishi mashariki mwa Jordan

Asheri, Isakari na Zabuloni walikuwa wana wengine wa Yakub. Benyamini alikuwa mwana mdogo na ndugu pekee kamili wa Yusufu.

Wana wa Yakub wote walimuamini  Mungu mmoja na walifuata dini ya Ibrahim (AS). Mwishoni mwa maisha yake, Yakub (AS) aliwaambia wanawe wafuate njia ya Ibrahim (AS):  "Je! Mlikuwapo yalipo mfikia Yaaqub mauti, akawaambia wanawe: Mtamuabudu nani baada yangu? Wakasema: Tutamuabudu Mungu wako na Mungu wa baba zako, Ibrahim na Ismail na Is- hak, Mungu Mmoja tu, na sisi tunasilimu kwake.” (Surat Al-Baqarah, Aya ya 133).

captcha