IQNA

Shakhsia katika Qur'ani/2

Hawa; Mama wa Mwanadamu

18:16 - July 26, 2022
Habari ID: 3475544
TEHRAN (IQNA) – Kwa mujibu wa Qur'ani Tukufu, Hawa ni Mama wa ubinadamu ambaye asili ya kuwepo kwake ni sawa na ile ya Nabii Adam (AS).

Mwenyezi Mungu, alimuumba Adam (AS) kwa udongo na kisha akamuumba mke wake kutokana na kiini hicho hicho.

Wanadamu wote wametokana na Adam (AS) na Hawa. Hawa ndiye mwanamke wa kwanza na mama wa ubinadamu. Qur'ani Tukufu inasema Adam (AS) alikuwa na mke lakini haitaji jina lake, "  Na tulisema: Ewe Adam! Kaa wewe na mkeo katika Bustani, na kuleni humo maridhawa popote mpendapo, lakini msiukaribie mti huu tu; mkawa katika wale walio dhulumu." (Surah Al-Baqarah, aya ya 35)

Katika Hadith na tafsiri za Qur'ani, jina lake limetajwa kuwa ni Hawa. Wafasiri wa Quran wanasema jina lake linatokana na neno Hayy (aliye hai) kwani yeye ndiye mama wa wanadamu wote walio hai.

Qur'ani Tukufu imefafanua juu ya kuumbwa kwa Adam (AS) kutokana na mchanga na udongo lakini haizungumzii maelezo ya uumbaji wa Hawa. Katika baadhi ya aya, Qur'ani Tukufu inasema Mungu alimuumba kwanza Adam (AS) na kisha mkewe (kutokana na udongo uliobaki). “Amekuumbeni kutokana na nafsi moja. Kisha akamfanya mwenziwe katika nafsi ile ile.” (Surah Az-Zumar, Aya ya 6)

Kwa hiyo Mwenyezi Mungu amewaumba wanadamu kutokana na nafsi moja. Wafasiri wengi wa Qur'ani wanaamini kwamba "nafsi moja" inarejelea Adam (AS) na mwenzi wake inamrejelea Hawa.

Katika Surah An-Nisa, pia, kuna aya inayosema Mwenyezi Mungu aliumba wanadamu wote kutoka kwa nafsi moja (Adam) na kwamba aliumba mke wa Adam kutoka kwa nafsi yake na kisha akaijaza ardhi kwa wanaume na wanawake wengi. Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi aliye kuumbeni kutokana na nafsi moja, na akamuumba mkewe kutoka nafsi ile ile. Na akaeneza kutokana na wawili hao wanaume na wanawake wengi..” (Surah An-Nisa, Aya ya 1)

Kila mtu ana mwelekeo wa kuwa pamoja na wale ambao ni wa aina yake na kwa hiyo, Mwenyezi Mungu alimuumba Hawa kutoka nafsi moja na ile Adam (AS). “Yeye ndiye aliye kuumbeni katika nafsi moja; na katika hiyo hiyo akamfanya mwenzi wake, ili akae naye kwa utulivu." (Surah Al-A’raf, Aya ya 189)

Baada ya kuumbwa kwao, Adam na Hawa wanaishi katika Janna  kwa amri ya Mwenyezi Mungu ambaye aliwataka watumie baraka zote katika Janna lakini wasikaribie mti hata mmoja. “Na tulisema: Ewe Adam! Kaa wewe na mkeo katika Bustani, na kuleni humo maridhawa popote mpendapo, lakini msiukaribie mti huu tu; mkawa katika wale walio dhulumu." (Surah Al-Baqarah, Aya ya 35)

Hata hivyo, Shetani aliwadanganya wote wawili na wanakula tunda lililokatazwa na hivyo wakati huo waliondoka katika Janna na kuelekea kuishi ardhini.

Katika Uyahudi na Ukristo, Hawa anatambulishwa kuwa ndiye aliyedanganywa kwanza na Shetani na kupitia kwake Shetani akamdanganya Adam. Katika Quran, hata hivyo, Adamu na Hawa wanawajibika sawa kwa kile kilichotokea: "  Lakini Shetani aliwatelezesha hao wawili na akawatoa katika waliyo kuwamo, na tukasema: Shukeni, nanyi ni maadui nyinyi kwa nyinyi. Katika ardhi yatakuwa makaazi yenu na starehe kwa muda. (Surah Al-Baqarah, Aya ya 36).

captcha