IQNA

Shakhsia katika Qur'ani Tukufu / 13

Hazrat Ibrahim na mitihani Migumu kutoka kwa Mwenyezi Mungu

14:14 - December 15, 2022
Habari ID: 3476252
TEHRAN (IQNA) – Ni sunna ya Mwenyezi Mungu huwajaribu waja wake na mitihani hii wakati mwingine ni rahisi na wakati mwingine migumu. Hakuna mtu mwingine ambaye angeweza kustahimili mitihani ambayo Mwenyezi alimpa Nabii Ibrahim (AS).

Hadhrat Ibrahim alikuwa katika kizazi cha Nabii Nuh. Kwa mujibu wa simulizi, alizaliwa yapata miaka 3,000 baada ya kuumbwa Adam au miaka 1,263 baada ya kuzaliwa Hadhrat Nuh.

Baadhi ya wanahistoria wanaamini Nabii  Ibrahim alizaliwa katika kijiji kiitwacho "Barzeh" karibu na Damascus ya leo na wengine wanasema alizaliwa Babeli ambayo ni Iraq ya leo.

Nabii huyu wa Mwenyezi Mungu alizaliwa wakati wa utawala wa Nimrodi. Mfalme huyo alikuwa ameamuru kuuawa kwa watoto wote waliozaliwa baada ya wanajimu kutabiri kwamba mvulana atazaliwa na kwamba atapinga ibada ya sanamu. Hii ndiyo sababu mama yake Hadhrat Ibrahim alimzaa kwa siri na katika jangwa.

Kuna maoni tofauti kuhusu baba yake Nabii Ibrahim. Baadhi ya wanahistoria wamemwita "Tarokh" au "Tarah" kama baba yake Agano la Kale linamwita "Tarah". Aya ya 74 ya Surah Al-An’am inasema  Na pale Ibrahim alipo mwambia baba yake, Azar: Unayafanya masanamu kuwa ni miungu? Hakika mimi nakuona wewe na watu wako mmo katika opotofu ulio wazi".

Aya hii hii imewafanya baadhi ya wafasiri kuhitimisha kwamba Azar alikuwa baba yake Hazrat Ibrahim. Ingawa baadhi ya wataalamu wengine wanasema Azar hakuwa baba bali mlezi wa Hadhrat Ibrahim.

Kuna marejeo 69 kwa Nabii Ibrahim katika Qur'ani Tukufu na Sura imepewa jina lake. Kitabu kinazungumzia utume wake na wito wake wa tauhidi. Hadhrat Ibrahim ana nafasi maalum kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu alimpa wadhifa wa Imamu baada ya kufaulu kupitia mitihani kadhaa. Hakuna nabii mwingine kabla yake aliyepata nafasi hii.

Qur'ani Tukufu pia inamtaja Hadhrat Ibrahim kama mfano wa kuigwa katika kutetea imani ya Mungu mmoja na kukabiliana na ibada ya masanamu. Kupoa kwa moto uliokuwa umuangamize na kuwarejeshea uhai ndege wanne waliokufa ni miongoni mwa miujiza ya nabii Ibrahim.

Yeye, pamoja na mwanawe Ismail, walipewa kazi ya kujenga upya Al-Kaaba. Kwa mujibu wa simulizi, eneo takatifu lilijengwa kwa mara ya kwanza na Hadhrat Adam na Hadhrat Ibrahim alilijenga upya.

Moja ya mitihani aliyopta Hadhrat Ibrahim kutoka kwa Mwenyezi Mungu ilikuwa ni ule ambao aliombwa kumchinja mwanawe, Ismail. Jukumu hili alipewa wakati wa moja ya ndoto zake na akaikubali. Ingawa nabii alikuwa amemleta mwanawe mahali pa dhabihu, Mwenyezi Mungu alikubali kujitolea kwake  kabla ya tendo la dhabihu kufanywa na badala yake akampa kondoo dume kwa ajili ya dhabihu.

Kwa mujibu wa Qur'ani Tukufu na maandiko mengine ya kidini, Hadhrat Ibrahim ni babu wa baadhi ya mitume waliokuja baada yake. Mwanawe Ishaq ni babu wa manabii wa Kiisraeli kama vile Yaqub, Yusuf, Dawud, Sulaiman, Ayyub, Musa na Harun.

Zaidi ya hayo, Hadhrat Maryam alikuwa dhuria wa Is-haq na Mtume Muhammad (SAW) alikuwa ni dhuria wa Ismail; ndio maana Hadhrat Ibrahim wakati mwingine anaitwa "Ab ul Anbiya" au baba wa Mitume.

Hadhrat Ibrahim aliishi kati ya miaka 175 hadi 200 na akazikwa kwenye shamba lake lililoitwa Hebron au Al Khalil ambalo sasa liko katika ardhi ya Palestina ambayo leo inakaliwa kwa mabavu na Wazayuni.

captcha