IQNA

Shakhsia Katika Qur'ani Tukufu / 14

Mbinu ya Mjadala aliyotumia Nabii Ibrahim (AS)

12:05 - November 10, 2022
Habari ID: 3476065
TEHRAN (IQNA) – Watu wenye kutumia akili na wenye kutegemea mantiki hutumia mijadala au midahalo kushawishi au kuwakinaisha mwengine kuhusu mitazamoa yao. Mfano wa kihistoria wa mijadala ambayo Nabii Ibrahim –Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake-(AS) alikuwa nayo na makundi tofauti.

Ibrahim (AS) aliishi wakati ambapo ibada ya sanamu ilikuwa imeenea lakini hakuwa na imani katika sanamu na alitumia kila fursa kuonyesha kwamba masanamu hayana uwezo wowote. Njia moja aliyotumia ni kufanya midahalo na majadiliano. Alikuwa na mijadala mingi na baba yake wa kambo, ambaye alikuwa mwabudu sanamu.

Baada ya kuharibu masanamu, alifanya mjadala na Nimrodi, mtawala wa wakati huo. Pia alikuwa na mijadala na waabudu jua, mwezi na nyota.

Ibrahim (AS) alitumia njia za ufanisi katika mijadala yake. Kwa mfano, alitumia maswali yenye akili ili kuvuta fikira za makafiri na waabudu masanamu. Alitumia njia za kimantiki kuwafahamisha kuhusu udhaifu na kasoro katika imani na matendo yao ya kuabudu sanami. Alimwambia hivi baba yake wa kambo: “ Ewe baba yangu! Kwa yakini imenifikia ilimu isiyo kufikia wewe. Basi nifuate mimi, nami nitakuongoza Njia Iliyo Sawa.” (Surah Maryam, Aya ya 43)

Pia aliuliza maswali ili kuwafanya waabudu masanamu watilie shaka imani yao na kisha akawafanya wakabiliane na makosa yao: “Akamwambia baba yake na watu wake: "Alipo mwambia baba yake na kaumu yake: Mnaabudu nini?  Wakasema: Tunaabudu masanamu, daima tunayanyenyekea. Akasema: Je! Yanakusikieni mnapo yaita? Au yanakufaeni, au yanakudhuruni?  Wakasema: Bali tumewakuta baba zetu wakifanya hivyo hivyo."  (Sura Ash-Shu’ara, Aya 70-74).

Katika mijadala yake, Ibrahim (AS) alitumia ulinganisho, hoja na njia nyinginezo kuwashawishi watu. Mojawapo ya mijadala yake mizuri ilikuwa ule na wale wanaoabudu nyota. Kwanza alijitambulisha kuwa mwabudu nyota lakini kisha akapinga imani hiyo na kufikia natija kwamba ni Mwenyezi Mungu tu, Mweza Yote, anayestahili kuabudiwa. “Na kadhaalika tulimwonyesha Ibrahim ufalme wa mbingu na ardhi, na ili awe miongoni mwa wenye yakini.  Na ulipo muingilia usiku akiona nyota, akasema: Huyu ni Mola Mlezi wangu. Ilipo tua akasema: Siwapendi wanao tua. Alipo uona mwezi unachomoza alisema: Huyu ndiye Mola Mlezi wangu. Ulipotua akasema: Kama Mola Mlezi wangu hakuniongoa, nitakuwa katika kaumu walio potea.  Na alipo liona jua linachomoza akasema: Huyu ndiye Mola Mlezi wangu. Huyu mkubwa kuliko wote. Lilipo tua, alisema: Enyi watu wangu! Mimi simo katika hayo mnayo fanyia ushirikina." (An'am, aya ya 75-78)

Katika mijadala yake, Ibrahim (AS) angetoa maoni yake kwa ujasiri bila woga wowote kuhusu vitisho na hatari lakini alitoa hoja zake kwa utulivu na amani na hii iliongeza ufanisi wa maneno yake.

captcha